Habari kamili: Magari yaliyogongana na kuvamia jengo la EXIM BANK Mwanakwerekwe Unguja

Magari mawili yaacha njia baada ya kugongana na kuvamia jengo la Exim Bank maeneo ya Raundiabauti Mwanakwerekwe na mmoja wa Askari aliyekuwa akilinda Bank hiyo kugongwa na kupata majeraha makubwa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamishna msaidizi wa Polisi Thobias Gesauda Sedoyeka amesema kuwa ajali hiyo imetokea Tarehe 8/10/2018 majira ya saa 11.15 Mchana huko mwanakwereke Wilaya ya Magharib B Unguja.

Amesema ajali hiyo ilihusishwa na gari yenye namba za usajili No. Z 254 GW P/V iliyokuwa ikiendeshwa na Pili Jumanne Shaaban mwenye umri wa miaka 34 Msangu wa Meli nne aliyoigonga gari kwa nyuma yenye No. za usajili Z 812 JL P/V iliyokuwa ikiendeshwa na Rafii Saidi Mnete mwenye umri wa miaka 38 mndengereko wa Polisi Ziwani, baada ya ajali hiyo gari hizo mbili ziliacha njia na kuelekea EXIM BANK Tawi la Mwanakwerekwe.

Kamanda Thobias amesema kuwa Baada ya kuacha njia gari yenye No. Z 812 JL P/V iligonga gari yenye No. Z  712 JG iliyoegeshwa nje ya Bank hiyo na gari Z. 254 GW ilimgonga Askari F.7607 PC Mwendambo Awesu Mwendambo miaka 35 Mshirazi wa FFU Mjini Magharib na baadae kugonga ukuta wa EXIM BANK Tawi la Mwanakwerekwe.

Hata hivyo Kamanda Thobias amethibitisha kuwa Askari aliepata ajali hiyo amepata majeraha makubwa katika mguu wa kushoto na michubuko mwilini huku gari zote zikiwa zimepata hasara kubwa.

Katika wiki hii Jumla ya ajali saba zimeripotiwa na moja imesababisha kifo napia kuna makosa ya usalama barabarani 326 yamekamatwa na  108 yamepelekwa Mahakamani na kutonzwa tozo ya Tsh. 3,899,000 kama niadhabu ya makosa yaliyofanywa.