Hakimu mkuu wa mahakama ya Shanzu mjini Mombasa, Patrick Odhiambo, amegonga nyoyo za Wakenya kwa kutumia busara kuamua kesi ambapo mshukiwa alikiri kosa la kuiba nywele bandia katika duka moja.

Mshukiwa huyo alimwambia hakimu kuwa umasikini ulimfanya ashindwe kujitunza vizuri, ndipo akajikuta ametumbukia kwenye wizi.

Ni wakati huo hakimu Odhiambo alitoa wito kwa mahakama kuchangia mshukiwa huyo kwa jina Chelagat, mwenye umri wa miaka 19, pesa ya kulipia nywele hiyo bandia aliyoiiba na vile vile kumchangia pesa ya kununua nywele zake na kumuepusha na kifungo cha miaka 2 gerezani.