Haya hapa majina ya Wafungwa 12 waliyoachiwa huru kwa msamaha wa Dkt. Shein Leo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wanafunzi kumi na mbili (12) ambao bado walikuwa wakiendelea kutumikia vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za Sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilieleza kuwa kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Rais Dk. Shein ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya Mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba wanafunzi hao waachiwe huru kuanzia tarehe 11 Januari 2019.

Taarifa hiyo, imeeleza kuwa, kwa kuwa Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo kesho tarehe  12 Januari 2019, na kwa kuwa Rais ameridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hii, wanafunzi hao waachiwe huru.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Mushtaki Mustafa Hashim, Ramadhan Abubakar Jabu, Bakari Khamis Juma, Maulid Kheir Suleiman, Othman Ramadhan Shija, Faiz Juma Faiz na Ali Haji Ali.

Aidha, wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni Suleiman Ali Suleiman, Ali Omar Ali, Ibrahim Mbarouk Omar, Mohamed Othman Ali na Mbarouk Ali Mbarouk.

Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi matukufu, huwahusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakisha muda mfupi wa kutumikia chuoni, wanaoonesha nidhamu nzuri chuoni na kujutia makosa yao.

Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa kama vile kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya Umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar