Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa mwanaye Dudley amepata maambukizi ya Virusi vya Corona ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwani tangu huu mwaka uanze hakuwa amesafiri kwenda nje ya nchi, ambapo dalili za awali ziligunduliwa na mama yake.

Mbowe aliyasema hayo kupitia taarifa ya familia yake kwa umma na Dunia nzima, amesema janga la Corona lipo mlangoni kwa kila mtu na huu siyo wakati wa malumbano na njia pekee ya kulishinda janga hilo ni kulikubali na kulikabili. 

“Hali ya Dudley sasa imeimarika, homa zimekwisha, bado yuko chini ya uangalizi maalum kwenye karantini, hatustahili kuchefuliwa na kejeli za Makonda, Rais wetu John Magufuli, unda timu ya kukusaidia na ushirikishe wadau wengine, wengi wako tayari kukusaidia CHADEMA tuko tayari kukusaidia na kulisaidia Taifa, siyo wakati wa kulumbana  huu” amesema Mbowe.

Aidha Mbowe amekiri kupata ushirikiano kutoka kwa Serikali kwa kufuatilia kwa ukaribu kwa wanafamilia na marafikiwaliokutana na mwanaye, na kusisitiza kuwa ugonjwa huo haupaswi kuwa siri japokuwa kuna miiko inayoongoza utoaji wa taarifa za wagonjwa na kwamba jukumu hili lisiachwe kwa Serikali pekee.