Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Serengeti mkoani Mara imemhukumu, Choral Samson (28) mkazi wa Burunga kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mama yake mzazi Rhobi Nyang’ombe (65).

Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Ismael Ngaile akitoa hukumu hiyo leo Jumatatu Machi 25, 2019 amesema mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Amesema hukumu hiyo inatolewa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Mapema mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Renatus Zakeo katika kesi ya jinai namba 8/2018 amesema mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 26, 2017 majira ya saa 3 usiku ambako alifanya mapenzi na mama yake bila ridhaa yake.

Ameomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ingawa hana rekodi ya makosa mengine.

Mshitakiwa ameomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni kosa la kwanza.