Hukumu kesi ya Mbunge Chadema kujulikana leo

Katibu Mkuu Chadema Dk Vicent Mashinji, mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa na katibu wake, Emmanuel Masonga wamewasili katika mahakama ya wilaya ya Mbozi, Songwe kusikiliza hukumu ya Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga.

Haonga na wenzake, Wilfredy Mwalusamba (katibu wake) na Mashaka Mwampashi wanakabiliwa na makosa matatu ya kufanya fujo na kuvuruga mkutano wa uchaguzi wa baraza la mji mdogo wa Mlowo,  kosa la pili na tatu ni kuwazuia  askari kutekeleza majukumu yao.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 28, 2017, na leo Ijumaa Agosti 10, 2018 mahakama hiyo inatarajia kutoa hukumu ya kesi hiyo.

Mbali na viongozi hao, pia wananchi na wafuasi wa Chadema wameanza kumiminika katika mahakama hiyo huku ulinzi ukizidi kuimarishwa kutokana na askari kutanda kila kona wakiwa na silaha za moto.