Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge leo Mei 23, 2019 itawasilisha bungeni taarifa ya shauri linalomhusu mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele la kulidharau Bunge, kugonganisha mihimili na utovu wa nidhamu.

Masele alihojiwa na kamati hiyo Jumatatu Mei 20 mwaka huu akituhumiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba amekuwa na utovu wa nidhamu pamoja na kutoa maneno ya kugonganisha mihimili.

Spika Ndugai alilieleza Bunge Mei 16 mwaka huu kwamba kutokana na utovu huo wa nidhamu amesimamisha uwakilishi wa Masele katika Bunge la Afrika (PAP) lililokuwa likiendelea nchini Afrika Kusini na kuagiza mbunge huyo kurejea nchini.

Alisema mara baada ya kurejea nchini, Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa PAP atahojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge pamoja na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM. Kamati zote hizo zimekwisha kumhoji.

Tayari taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka Bunge imewasilisha leo Alhamisi bungeni na Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Almas Maige ambapo itasomwa baadaye.