Huyu hapa Rubani Kijana Kutoka Tanzania


Rubani kijana kabisa katika Kampuni ya Ndege la Tanzania (ATCL)
Simon Myagila mwenye umri wa miaka 26 ambaye ni miongoni mwa marubani wa ndege mpya za Airbus A220-300 nchini.

Pamoja na kurusha ndege hizo, pia alikuwa miongoni mwa marubani waliorusha mbawa hizo za Mlima Kilimanjaro kutoka nchini Canada hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Najua hatuzungumzii ukabila, tunajivunia utanzania wetu, lakini kwa asili kabila langu mimi ni Mpogoro,” anasema rubani huyo wa ATCL.

Amesema alianza kazi hapo kwa kurusha ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba idadi ya watu mpaka 76. Alianza safari yake ya urubani mwishoni mwa mwaka 2014 baada ya kuhitimu Kidato cha Sita. Kwa wakati huo, alifanikiwa kupata chuo katika Jimbo la Florida nchini Marekani ambako alianzia leseni ya mwanzo ya urubani ya PPL baadaye IR pamoja na CPL, na kuhitimu.


Simon Myagila alirejea nyumbani Mei mwaka 2016, na mwaka mmoja baadaye, Mei mwaka 2017 alipata nafasi ATCL na kuwa miongoni mwa marubani wanne waliochaguliwa kwenda Toronto kwa masomo ya kurusha Bombardier Q400, ndege mpya za kwanza zilizonunuliwa na Serikali ya Rais John Magufuli. Mafunzo hayo ya mwezi mmoja yalimpa uwezo wa kurusha ndege hizo hapa nchini na hivyo kuwa miongoni mwa marubani wanaoziwezesha kuwa angani ndege hizo nchini.

Agosti mwaka huu, alifanikiwa tena kupata nafasi ya kwenda mafunzoni kwa ajiri ya ndege mpya kabisa na ya kisasa ambayo ni ya kwanza Afrika nzima ya Airbus A220-300.

Amesema anaona fahari kulitumikia taifa na hasa namna ambavyo nchi inajizatiti kuinua utalii kupitia kuwa na shirika la kisasa la ndege ili kuwapeleka watu maeneo mbalimbali yenye vivutio kwa kasi.

Chanzo Habari leo.