Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita ni siku ambayo haitasahaulika kwani siku hio Tanzania ilimpoteza nguli wa filamu Tanzania Marehemu Steven Kanumba ambae aliitangaza nchi katika mataifa mbalimbali kupitia uigizaji wake

Steven Charles Kanumba alikuwa msanii wa maigizo na filamu kutoka nchini Tanzania alizaliwa tarehe 8 Januari 1984, Mkoani  Shinyanga, Baba yake alikuwa anaitwa Charles Kanumba  na  mama yake aliitwa Flora Mutegoa.

Steven kanumba  Alianza elimu yake ya msingi katika shule ya Bugoyi Primary School na aliendelea na elimu ya sekondari katika shule iliyoitwa Mwadui Secondary School, Na baadae alihamishiwa Vosa Mission Secondary School . Alijiunga kidato cha 5 &6 katika Shule ya Sekondari Jitegemee iliyopo jijini Dar-es-salaam

Kanumba alianza kuigizakwenye miaka ya 1990 ambapo alianza kufahamika zaidi mwaka 2002 mara tu baada ya kujiunga na kundi la sanaa ya maigizo maarufu kama Kaole Sanaa Group .

Alijibebea umaarufu mkubwa nchini Tanzania na alikuwa kipenzi cha wengi na alikubalika karibia nchi zote za Afrika Mashariki na maziwa makuu.

Kanumba Aliweza kutangaza sanaa nchi za Afrika ya Magharibi ikiwemo  Nigeria na pia Wanigeria walipendezewa na uigizaji wake hivyo kushirikiana pamoja naye katika filamu kadhaa kama vile Dar to Lagos pamoja na She is My Sister .

Marehemu Kanumba alikuwa  ni msanii wa kwanza kufanya kazi nje ya Nchi na kuvutia wasanii wa nje kuja kuigiza nchini Tanzani pia ameweza kuwaleta waongozaji filamu kadhaa wa Kinigeria nchini.

Kanumba alifariki dunia tarehe 07/04/ 2012 na Alizikwa katika makaburi ya kinondoni chanzo cha kifo chake inasemekana alipata jeraha kichwani kwa kile kilichodaiwa aligongwa na rafiki yake wa kike ambapo alipelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa mahututi  na baada ya vipimo madaktari walithibitisha kwamba kifo chake kilitokana na jeraha kwenye ubungo kumsababishia kukosa pumzi na kufariki.

Huyu ndio Steven Charles Kanumba ambae mpaka sasa bado watanzania wanamlilia tutamkumbuka kwa yale mengi mazuri aliyotuachia Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi – Amin