Maambukizo ya virusi vya corona yamepindukia milioni 39 ulimwenguni, huku watu milioni 1.1 wakipoteza maisha, kufikia jioni ya jana, Ijumaa. Marekani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu milioni nane, walioambukizwa maradhi ya COVID-19. Chuo Kikuu cha John Hopkins, kimesema kwamba kufikia jioni ya jana, Marekani ilikuwa imeshapoteza watu 218,000, kutokana na maradhi hayo.

Inayofuatia kwa maambukizo mengi duniani ni India, ambako watu milioni 7.4 wameambukizwa, na kisha Brazil, iliyosajili hadi sasa watu milioni 5.1. Kilimwengu, jana peke yake walisajiliwa watu 400,000 walioambukizwa, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la AFP. Hapa barani Ulaya, idadi ya maambukizo mapya ya kila siku imevuuka asilimia 44 kwa wiki moja, ambapo watu 121,000 wamesajiliwa kuambukizwa, virusi hivyo vya corona.

Mataifa kadhaa ya Ulaya yameanza tena kuchukuwa hatua, za kukabiliana na kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo, ikiwemo kufungwa mikahawa, maduka, na maeneo ya wazi. Ujerumani kwa upande wake, imethibitisha watu wengine 7,830 walioambukizwa virusi hivyo ndani ya masaa 24 yaliyopita, huku wengine 33 wakipoteza maisha. Jumla ya maambukizo hapa Ujerumani sasa ni 348,557, kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch.