Maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa Jayalalithaa Jayaram, mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini India.

Mkuu huyo wa serikali ya jimbo la Tamil Nadu alipatwa na mshtuko wa moyo Jumapili usiku na akafariki saa 23:30 (18:00 GMT) siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa hospitali ya Apollo, mjini Chennai.

Mwili wake, ukiwa umevikwa bendera ya India, umewekwa kwa ajali ya kutazamwa na umma katika ukumbi mkubwa katika makao makuu ya jimbo hilo.

Polisi wa ziada wametumwa kudhibiti waombolezaji na kushika doria huku kukiwa na wasiwasi wa kuzuka kwa fujo.

Alikuwa anaenziwa sana na wafuasi wake, baadhi ambao walikuwa wanamwita “Amma” (mama) na kuna wasiwasi kwamba huenda baadhi wakaamua kujidhuru au kuzua ghasia.

Awali, baada ya taarifa za kifo chake kutangazwa, kulitokea makabiliano kati ya polisi na wafuasi wake nje ya hospitali hiyo ya kibinafsi ya Apollo. Taarifa hizo baadaye ziliondolewa, ingawa saa chache baadaye alithibitishwa kufariki.

Baadhi ya wafuasi wake wamekuwa wakilia hadharani na kujipiga vichwa na vifua hivyo kumetangazwa siku saba za maombolezi katika jimbo lake la  Tamil Nadu.

Serikali kuu mjini Delhi nayo imetangaza Jumanne kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa kama heshima kwake.

Waziri Mkuu Narendra Modi atahudhuria ibada ya mazishi ya kiongozi huyo ambayo yatafanyika baadaye Jumanne.