Mpango wa kuanzisha magari ya kutumia nyaya kukwea Mlima Kilimanjaro umechukua sura mpya baada ya mawaziri wawili husika nchini Tanzania kupishana kauli mitandanoni.

Mpango huo ulitangazwa mwezi Aprili na Waziri wa Utalii wa nchi hiyo Hamisi Kigwangalla ili kukuza maradufu idadi ya watalii wanaoukwea mlima huo na kuongeza pato la taifa hilo ambalo linategemea kwa kiasi kikubwa sekta hiyo.

Hata hivyo, kumekuwa na mashaka juu ya hali ya kimazingira katika mlima huo endapo magari hayo yatakubaliwa kufanya kazi.

Mwishoni mwa juma, Waziri wa Mazingira wa Tanzania, January Makamba aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa ofisi yake ndiyo itakayotathmini hali ya kimazingira kabla ya kutoa kibali kwa ujenzi wa mradi huo.

Kigwangalla alijibu kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa ‘watu wa Mazingira wanataka kuingilia mradi’ huo.

Watu wa mazingira wanataka kuingilia kati mradi wa cable cars KILIMANJARO. Lengo letu ni kukuza utalii, kuongeza mapato na kuboresha experience ya watalii wetu nchini. Tusipokuwa wabunifu tunatukanwa kutokutumia vizuri vivutio vyetu, tukiamka wanakuja ‘speed governors’.

Ujumbe huo ulifungua ukurasa wa ‘vita ya maneno’ baina ya mawaziri hao na kuchagizwa na mamia ya watu wanaowafuatilia katika mtandao huo.

Kigwangalla aliendeleza ‘mashambulizi’ kwa wizara hiyo: “Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake?Hizi haziharibu mazingira? Cable inapita juu inaharibu mazingira gani? Zaidi ya ekari 350,000/- za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? ‘Watu wa mazingira’ wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu?”

Hivi kuna nchi ngapi zimeweka cable cars kwenye milima yake?Hizi haziharibu mazingira? Cable inapita juu inaharibu mazingira gani? Zaidi ya ekari 350,000/- za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? ‘Watu wa mazingira’ wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu?

Mlolongo wa regulative mechanisms zimeua biashara zetu na kukwamisha uwekezaji kwa muda mrefu sana hapa nchini. Hivi sasa tunajaribu kuondoa vikwazo ili kukuza uwekezaji na uchumi wetu. Nchi zinazokua kwa kasi zimeepuka sana njia hizo za kimagharibi.

Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo wa kijamii, kwa dhihaka wakamwandikia Makamba ‘wapunguze makongamano.’

Hilo likamwibua Makamba ambaye alidai kuwa maelezo yake ndivyo ambavyo sheria inaelekeza na kusema hawezi kubishana hadharani na waziri mwenzake.

“Baada ya kuona hilo jambo kwenye blogu, nikaeleza kile sheria inachotaka. Itakuwa ni jambo la kitoto kwangu, kumjibu, kujibizana ama kumshambulia waziri mwenzangu ambaye anataka kuboresha mambo kwenye sekta yake,” aliandika Makamba.

Kigwangalla baadae akaandika kuwa alilazimika kulijibia suala hilo mitandaoni kwa sababu liibuliwa mtandaoni, na kuwa toka hapo wasingeweza kukamilisha mradi huo bila kufanyika kwa tathmini ya mazingira.

Wao wametweet, hawakuleta barua. Majibu ya swala la kwenye mtandao yanatolewa mtandaoni. Kwani unadhani sisi tungefanya mradi huu bila kuangalia sheria za mazingira? Mlima tumehifadhi wenyewe miaka yote, saa 24, leo tufanye kitu cha kuuharibu? Ama ni dharau na kujionesha tu?

Kuna hekima, busara na unafiki. Saa nyingine kukaa kimya ni busara ama ni unafiki. Sikuwahi kujifunza unafiki maisha yangu. Hupenda kuwa wazi. Nimekasirika utajua, nimefurahishwa utajua. Hekima ni kutenda mema/sawa hata ukiwa peke yako chumbani siyo kujifanyisha ili uonekane!

Makamba mwishowe akawaasa watu kuacha kuendelea kuzungumzia na kupalilia jambo hilo mtandaoni kwani wote wanajenga nyumba moja: “…naomba hili jambo sasa liishe. Tunajenga nyumba moja, ya Watanzania. Hii ni kazi ya umma, na ya kupita. Leo upo, kesho haupo. Tulipoghafirika tumesameheana.”

Ndugu yangu, naomba hili jambo sasa liishe. Tunajenga nyumba moja, ya Watanzania. Hii ni kazi ya umma, na ya kupita. Leo upo, kesho haupo. Tulipoghafirika tumesameheana. Sasa tutazame mpira, na baadaye

Takriban watalii 50,000 hupanda mlima Kilimanjaro kila mwaka.

Wote hao wanakwea mlima huo mrefu zaidi barani Afrika kwa miguu, hivyo lazima awe ni mwenye afya njema.

Wizara ya Utalii nchini Tanzania inaamini kwa kuanzisha njia mpya ya kupandisha watu kileleni, idadi ya watalii wanaozuru kivutio hicho itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.

”Gari la kutumia nyaya linaweza kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 50 kupitia kuwawezesha wale wasioweza kupanda mlima huo kwa miguu,” Constantine Kanyasu alilieleza Shirika la habari la Reuters mwezi Mei.

Watoa huduma za kitalii walilia pendekezo la kuidhinishwa magari ya umeme Mlima Kilimanjaro.

Kuna kampuni mbili, moja kutoka Uchina na nyingine ya Kimagharibi ambazo tayari zimeshaonesha nia ya kuwekeza kwenye mradi huo.

Hata hivyo, wapagazi na watu wengine wanaojishughulisha na biashara ya utalii kwenye mlima huo wanapinga mpango huo wakidai utawanyima biashara.

Loishiye Mollel, ambaye ni kiongozi wa shirika la wachukuzi wa mizigo, amesema kuwa wageni hutumia wiki moja kupanda mlima huo.

”Mgeni mmoja kutoka Marekani anaweza kuandamana na takriban watu 15 nyuma yake , huku watu 13 wakiwa wachukuzi, mpishi na mwelekezi . Kazi zote hizo zitaathiriwa na magari ya nyaya”, alisema.

‘Tunapendekeza kwamba mlima huu uwachwe vile ulivyo”.

Kuna takriban wachukuzi 20,000 wanaofanya kazi kati ya mlima Kilimajaro na Meru.

Chanzo: BBC Swahili.