Je Membe ataungana na Lowassa, Sumaye kumdondosha Rais Magufuli uchaguzi 2020?

Jina la Bernard Camilius Membe ambaye amewahi kuwa waziri wa mambo ya nje kwa miaka 8 katika serikali ya Jakaya Kikwete limekuwa likigonga vichwa vya habari nchini Tanzania.

Tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu CCM, Dkt. Bashiru Ally kuwa Membe amekuwa na mwenendo wa kutia shaka ndani ya chama hicho na kumtaka afike ofisi za chama hicho jijini Dar es salaam kujitetea na tuhuma zinazomkabili.

Siku chache baadaye Membe alijitokeza na kutoa taarifa kupitia kundi sogozi ambalo mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa wanachama wake na alisoma ujumbe huo.

Membe alieleza kuwa atakwenda ofisini kwa Katibu Mkuu wa CCM iwapo atahakikisha anamwita mtu aliyechapisha tuhuma dhidi yake.

Duru za ulinzi na usalama zinabainisha kuwa kwa sasa Membe ni mshauri wa masuala ya usalama wa rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa tangu alipochukua madaraka mnamo Desemba 2017 kutoka kwa Robert Mugabe.

Kitendo cha kutajwa jina la Membe katika kinyang’anyiro cha mwaka 2020 ikiwa ni katikati ya uongozi wa Rais Magufuli kinafanishwa na kile kilichowahi kutokea kwa Edward Lowassa na Gharib Bilal katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Ikiwa ni miaka miwili baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alitajwa kuwa kwenye mikakati ya chini chini kupambana na Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi ndani ya CCM mwaka 2010. Hata hivyo Kikwete alipitishwa na kushinda, lakini Lowassa hakugo,mbea ndani ya chama.

Naye mwanasiasa mkongwe visiwani Zanzibara, Dk. Gharib Bilal alijitokeza ndani ya CCM kwa upande wa Zanzibar akitaka kumrithi Amani Abeid Karume, mtoto wa rais wa kwanza visiwani humo, Abeid Karume.

Lowassa na MagufuliBaada ya Lowassa (kulia) kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha CCM alihamia Chadema na kushindana tena na Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa 2015.

Ikumbukwe, wakati Bilal akijitokeza, Karume alikuwa ametumikia miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa visiwani humo.

Kwa mujibu wa desturi za uongozi ndani ya CCM, rais aliyeko madarakani huachiwa aendelee na nafasi hiyo awamu ya pili bila kupingwa ndani ya chama.

Kwa Lowassa naye alitaka kwenda kinyume cha desturi za CCM kwa kupambana na rafiki yake kipenzi wa zamani Jakaya Kkwete, ambaye alikuwa amemaliza miaka mitano ya kwanza kama rais nchini Tanzania.

Mnamo Julai 12, 2015 baada jina lake kukatwa mapema chini ya uenyekiti wa Jakaya Kikwete ndani ya CCM, Edward Lowassa aliamua kuchukua uamuzi mgumu kwa kuhamia Chadema kisha kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani, Ukawa.

Utaratibu wa CCM ni kwamba kila rais anayeoomba mara ya pili kuendelea na wadhifa huo, huwa hapingwi. Kwamba hakuna mwanachama mwingine anayejitokeza kupambana nae.

Kwahiyo iwapo Membe ataamua kuachana na CCM jambo linalofikiriwa sasa ni kuhamia Chadema ambako yuko hasimu wake kisiasa, Edward Lowassa.

Mwaka 2015 Lowassa alipoamua kuhama CCM kwenda upinzani baada ya kushindwa kufurukuta kwenye kinyanyiro cha kuwania uteuzi ndani ya chama hicho, alitikisa nchi.

Ni mwaka 2015 ndiyo ulishuhudia mawaziri wakuu wawili wastaafu Lowassa na Frederick Sumaye wakiamua kukihama chama tawala CCM na kwenda upinzani. Na sasa Bernard Membe anaweza kutumia kigezo hicho na kuhamia upinzani kasha mwaka 2020 akawa mgombea wao.

Ikumbukwe, Sumaye na Lowassa walikuwa wanasiasa wasioiva chungu kimoja, lakini mwaka 2015 wote walihamia Chadema. Hivyo kumaliza misuguano ya muda mrefu.

Mmembe na ClintonMembe amehudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwa miaka minane. Pichani akimkaribisha Tanzania aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton Juni 11, 2011.

Kwa upande wa Lowassa na Membe walikuwa miongoni mwa majabali wa kisiasa walioshindana ndani ya CCM.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa kambi mbili za Lowassa na Membe zilikuwa na uhasama mkubwa kuanzia ndani ya jumuiya za Chama tawala CCM.

Uhasama wa pande mbili hizo ulichochea vita kubwa ya madaraka kuelekea mwaka 2015. Lakini jina la Lowassa lilikatwa katika hatua za awali, huku Membe akitinga katika tano bora ambapo majina yao yalipigiwa kura.

Hata hivyo nalo jina la Membe lilikatwa katika hatua hii. Mwishowe John Magufuli akateuliwa.

Swali moja kuu hadi sasa, je Membe ataweza kuchukua uamuzi kama wa Lowassa kuhamia upinzani? Vyama vya upinzani ambavyo ni maarufu kwa sasa ni Chadema, Cuf na ACT Wazalendo vitakuwa tayari kuungana au kila kimoja kuwa na mpango wa kumpokea Membe kujiimarisha?

Tafsiri ya suala hili ni kwamba kadiri miaka inavyokwenda ndivyo wanasiasa ndani ya CCM wanaibuka kila mara kutamani kupambana na rais anayetakiwa kupitishwa bila kupingwa.

Hii ina maana desturi iliyopo CCM haizuii na wala sio sheria ambayo inakataza wanachama wao kumpinga rais anayetarajiwa kuomba mara ya pili. Ndiyo kusema CCM wanatakiwa kubadilika kama wanahitaji kumlinda rais aliyepo madarakani pale anapoomba awamu ya pili ndani ya chama chao.

Vinginevyo utaratibu wa sasa kuwa ni ‘uungwana’ tu kwa wanachama kumwachia rais John Magufuli kuomba tena mwaka 2020 bado hauwanyimi haki wanachama wa CCM kupambana na rais anayeomba ngwe ya pili.

Vilevile CCM wanatakiwa kuruhusu demokrasia ya kuwaachia wanachama hao washindane na rais aliyepo madarakani kama wanadhani kuzuia kisheria ni kibinya haki. Iwapo kuzuia kisheria ni kubinya haki, basi kuwaruhusu wanachama kuchuana na rais anayeomba ngwe ya pili liwe jambo halali na linalokubalika bila mizengwe.

Kama wanasiasa Lowassa, Membe, na Dk. Bilal wametajwa kujaribu kupambana na rais aliyepo madarakani, ni kwa vipi wanachama wengine ndani ya CCM, hawawezi kutumia waliotangulia kama mfano wao wa kuomba ridhaa kupambana na rais anayeomba awamu ya pili?

Chanzo BBC.