WAKATI dunia inapoadhimisha siku ya watu wenye ulemavu Disemba 3 ya kila mwaka, yatupasa tukumbuke kuwa hao ni binadamu kama sisi na haifai kuwadhihaki kwa namna yoyote ile.

Siku hii imeteuliwa na Umoja wa Mataifa maalumu kwa ajili ya kutambua nafasi ya watu wenye ulemavu, hadhi yao na haki wanazostahiki kupatiwa katika serikali za nchi zao, jamii, familia na jumuiya mbalimbali.

Leo nimeamua niliseme jambo moja ambalo sio zuri na mara nyingi hufanyiwa watu wenye ulemavu wa akili hasa watoto na vijana wanapokuwa mitaani.

Kwa bahati mbaya sana, miongoni mwa watendao hayo ni watu wazima ambao kimsingi wanapaswa kuwa wakemeaji kwa vijana wanaowakejeli watu ambao hawakupenda kuwa na kasoro za maumbile bali imetokea hivyo kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Kitendo hicho ni kile cha kuwapigia muziki watoto wenye ulemavu wa akili na kuwataka wacheze huku wanaowashawishi kufanya hivyo wakiwarikodi kwa simu zao.

Kwa kuwa hawajui wanachokifanya, na tabia yao ni kuwa watu wa kufurahi na kufurahisha, watoto hao hukubali kucheza muziki kwa mitindo tafauti huku mashabiki wanaowazunguka wakipiga kofi na kushangiria kwa vicheko.

Unaweza kupita mtaani ukawakuta kundi la vijana wamemzunguka mtoto mwenye ulemavu wa akili wakimpigia nyimbo za wasanii mashuhuri kama vile Nasib Abdul ‘Diamond’, Harmonize, Aslay na wengineo, huku masikini mtoto huyo akinengua.

Wakati huo, mabarobaro hao huwa wameshughulika kumrikodi kwa video wakitumia simu zao za mikononi.

La kusikitisha zaidi, furaha ya vijana hao hutimu kwa kuzirusha video hizo wanazowarikodi watoto wenye ulemavu wa akili hali inayowafanya waonekane kama kiburudisho au kichekesho cha watu wengine katika mitandao.

Hivi watu hawa hawaoni furaha nyengine zaidi ya kuwasumbua watoto wetu hao ambao kwa kweli wanahitaji marafiki lakini sio wa kutumia upungufu waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kujifurahisha nafsi zao?

Hebu mtu ajiulize iwapo ana ndugu au mtoto wake mwenye maumbile kama hayo atafurahi kumkuta akifanywa ‘Karagosi’ wa mtaa?

Kwa kuwa hakuna binadamu hata mmoja anayejua majaaliwa yake ya kesho, ni lazima tufike pahala kama wana jamii, vyombo vya Serikali, jumuiya za kiraia, viongozi wa dini na wanafamilia tujue dhambi tunayoifanya kwa kuwanyanyapaa watoto kama hao.

Na kwa kuwa mtu hajui mtoto atakayemzaa kesho, keshokutwa na mtondogoo atakuwa na hali gani, si vyema kuwageuza watoto wenye ulemavu wa akili kama kichekesho kwa kuwachezesha ngoma, kuwarikodi na kuwarusha mitandaoni.

Lazima tufahamu kuwa pamoja na mja wa Mungu kuzaliwa akiwa mlemavu, au akipata ulemavu baadae kwa sababu mbalimbali, bado anastahili heshima, thamani na haki za kimaisha kama wanazopata watu wengine.

Kwa kuwa sote twaweza kuwa ni ‘walemavu watarajiwa’, haifai kuwabughudhi na kuwakejeli wenzetu hao, na ndio maana Serikali za mataifa zimekuwa zikitunga sera na miongozo mbalimbali inayosisitiza umuhimu wa kuwajengea ustawi watu wenye ulemavu na kuwapa haki zao za msingi.

Halikadhalika, kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, sheria namba 11 inaeleza wazi usawa wa watu wote ikiwemo wenye ulemavu.

Ibara ya 11 (1) inaainisha kuwa watu wote wamezaliwa huru na sawa, na pia kifungu (2) kinaeleza kuwa, kila mtu anahaki ya kutambuliwa na kuheshimiwa utu wake.

Kama hiyo haitoshi, katika maazimio ya kimataifa juu ya haki za binadamu (UDHR), kifungu cha kwanza kinaeleza; “Binadamu wote wamezaliwa wakiwa sawa katika utu na haki, na wametofautiana kwa sababu maalumu tunapaswa tuishi kama ndugu”.

Tuwachukulie watu wenye ulemavu, iwe wa akili au mwenginewe, kuwa ni binadamu kama sisi ‘tunaojiona’ tumetimia, kwani wao hawakuchagua kuwa hivyo na hakuna anaependa azaliwe akiwa na upungufu.

Na Salum Vuai,

Baruapepe: salumss@yahoo.co.uk