Jeshi la Polisi lakanusha madai ya mtoto kufungiwa kabatini

Wakati binti wa kazi akieleza jinsi mwanaye mwenye umri wa miezi mitano alivyofungiwa kabatini na mwajiri wake mkoani Dodoma tangu alipozaliwa, Jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha madai ya mtoto huyo kufungiwa kabatini, na kusema kuwa mtuhumiwa wanamshikilia kwa usalama wake.

Akizungumza na eatv.tv,  Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilles Muroto amesema polisi wamefanya upekuzi katika nyumba ya mwajiri wa binti huyo ambaye ni mwalimu, Anitha Kimaro (46) na kubaini kuwa hakukuwa na kabati nyumbani kwake, na kukiri binti huyo ameshambuliwa na mwajiri wake.

Kesi ya shambulio ipo na ameshambuliwa kweli na ndiyo maana tunamshikilia. Anashikiliwa kutokana na usalama wake kwani kelele za watu ni nyingi, ila hili suala la kuwekwa mtoto kabatini halipo, uchunguzi wa kina unafanyika na kwamba lazima mwalimu huyo atafikishwa mahakamani ” amesema Muroto.

Binti huyo wa miaka 15,  akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alidai kufanyiwa ukatili kwa kupigwa na kufanyishwa kazi hadi usiku wa manane na bosi wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu na kwamba amekuwa akimwambia amfungie hadi usiku mtoto wake na kila alipovunja masharti alikumbana na kipigo.