Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo imekosoa kanuni za Baraza la Sanaa Taifa (Basata) za mwaka 2019 ambazo pamoja na mambo mengine zinaainisha kufungiwa maisha kwa msanii kujishughulisha na shughuli za sanaa kwa atakayebainika kuvunja kanuni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Andrew Chenge amesema hayo leo Ijumaa Februari 8, 2018 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo bungeni jijini Dodoma.

Chenge amesema kamati inaona kuwa kanuni na adhabu hizo ni kubwa na hazina uhalisia iwapo mtu atakiuka masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa kanuni hizo.

Ametoa mfano kanuni ya 64 inayosema msajiliwa au mtu yeyote kutozwa faini ya papo kwa papo isiyopungua Sh1milioni, kufungiwa kazi husika na kutozwa faini ya papo kwa papo isiyopungua Sh3milioni  au kuzuiwa kujishughulisha na kazi za sanaa maisha kwa kubainika kulingana na ukubwa wa kosa.

Amesema kanuni ya 64 haijaweka bayana kila kosa na adhabu inayostahili kuchukuliwa kwa atakayekiuka masharti ya kanuni hizo, badala yake adhabu zote zimewekwa kwa ujumla na zinaweza kutolewa pamoja .

Amesema kamati inaona kuwa adhabu zilizowekwa na kanuni ikiwepo ile ya kumfungia maisha msajiliwa kujihusisha na shughuli ya sanaa itasababisha vijana wengi kushindwa kuendesha maisha yao ya kila siku.

“Hivyo kamati iliona kuwa adhabu zilizowekwa na kanuni ikiwemo ile ya kumfungia maisha msajiliwa kujishughulisha na shughuli ya sanaa itasababisha vijana wengi kushindwa kuendesha maisha yao ya kila siku,” amesema Chenge.

“Na inaweza kusababisha vijana wengi kuingia katika makundi ya utumiaji wa dawa au hata kushiriki katika vitendo vingine vya uhalifu ili kuendesha maisha yao.”