Kamati ya Usimamizi wa Masuala ya Fedha ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (PAC) imetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ili kuisaidia serikali katika kudhibiti mapato ya serikali zisipotee.

Akifungua semina ya siku nne ya kamati hiyo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nnje kidogo ya Mji wa Zanzibar ,Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Khalid Salum Muhammed amesema wajumbe wa kamati hiyo watakapo zifahamu sheria mpya za fedha na Ununuzi zitasaidia ukusanyaji wa mapato.

Amesema Uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia 7.1 ambapo ukuwaji huo unatokana na usimamizi mzuri wa fedha zinazotokana na vyanzo vya mapato vya ndani na kusababisha serikali kupunguza utegemezi.

Hata hivyo amesema kutokana na uchumi wa Zanzibar kuimarika siku hadi siku ni vyema Kamati hiyo kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano pamoja na kuendelea kuchunguza hisabu za serikali ili ziweze kutumika kwa mahitaji yaliokusudia katika maendeleo ya Nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Masuala ya Fedha katika Baraza la Wawakilishi  Miraji Khamis Mussa amesema watahakikisha wanayatumia mafunzo watakayo yapata katika kuishauri serikali namna ya kutumia vyema fedha zinazopatikana.

Aidha amesema kamati hiyo pia imekusudia kupitia sheria mpya ya Fedha na ununuzi ili ziweze kufanya kazi kwa mahitaji yaliokusudia katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Mafunzo hayo ya siku nne kwa wajumbe wa kamati ya PAC ya baraza la Wawakilishi yamekusudia kupitia sheria mpya mbili zilizopitishwa ikiwemo Sheria ya ununuzi na uendeshaji wa mali za umma.

Na:Fat hiya Shehe Zanzibar24.