Kanda ya video yaonyesha mwandishi alivyopigwa na polisi Tanzania

Kanda ya video inayoonesha maafisa wa polisi wa Tanzania wakimpiga mwandishi wa habari imesambazwa kwa wingi katika mitandao ya kijamii.

Kanda hiyo ya dakika moja na sekunde ishirini inawaonyesha maafisa wa polisi wakimpiga mwandishi wa kituo kimoja cha redio na mbao na kumpiga mateke hadi akaanguka.

Kisa hicho kilitokea siku ya Jumatano katika uwanja wa michezo jijini Dar es Salaam baada ya mechi ya soka kati ya klabu ya Simba ya Tanzania dhidi ya klabu ya Asante Kotoko ya Ghana.

Bwana Mbise anasema kuwa tatizo lilianza baada ya maafisa wa polisi kujaribu kuwazuia waandishi kutoingia katika mkutano na waandishi wa habari licha ya kuwa na vitambulisho vyao.

”Walikuwa wakituzuia kutohudhuria tulipouliza kwa nini walianza kutusukuma nyuma. Niliwaambia wafanye kazi yao kwa utaalamu na watuwache tufanye kazi yetu na hivyo ndivyo waliponilenga mimi na kuanza kunipiga”, bwaa Mbise alisema.

Alipata majeraha ya mgongoni na mbavu.

Kamanda wa polisi wa jiji la Dar es salaam alipoulizwa kuhusu kisa hicho alisema kuwa yuko katika mkutano.

Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limetoa taarifa likisema: TFF imeshangazwa na inashutumu shambulizi hilo lililofanywa na maafisa wa polisi dhidi ya mwandishi wa habari wa maswala ya michezo Silas Mbise.

Kituo kimoja cha redio kimesambaza kanda ya shambulio hilo la polisi.