Wakulima wa zao la karafuu kisiwani Pemba wameiomba serikali ya mapinduzi Zanzibar kuchukua hatua za tahazari mapema  kukabiliana na wanunuzi wa karafuu mbichi  pamoja na wizi wa zao hilo ili kunusuru kutokea kwa  vifo visivyo tarajiwa kwa wakulima hao.

Ombi hilo limetolewa na Suleiman Mohd Khalfan ambaye ni mkulima wa zao hilo mbele ya Mkurugenzi muendeshaji wa shirika labiashara ya Taifa Zanzibar  ZSTC Dr. Said Seif Said alipokua katika ziara ya siku moja kisiwani Pemba ya kukagua jinsi hali ya uzaaji wa karafuu ulivyo na matayarisho ya uvunaji  kwa mwaka 2017 na 2018.

Suleiman amesema  kutokana na tamaa iliyojengeka kwa kwa baadhi ya watu juu ya zao hilo  kumekua kukijitokeza matendo mbali mbali ya kihalifu ambavyo hufanyiwa wakulima pamoja na wamiliki  pindi wanapokwenda kulinda mashamba yao jambo ambalo limepelekea hofu kubwa juu ya maisha yao.

Amesema  hadi sasa karafuu zinaonekana kuanza kuchumwa baadhi ya maeneo ya kisiwa cha Pemba lakini serikali za mitaa pamoja na vyombo vya ulinzi hawajaweka mikutano na wakulima  kuwaeleza vipi wamejipanga kuwadhibiti wizi pamoja na kuwahakikishia usalama wao na mali zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi muendeshaji wa shirika hilo Dr. Said Seif Mzee amesema  shirika limejipanga kwa  kununua vifaa vyote muhimu kama pishi, majamvi, magunia na kuwapatia mikopo wakulima ili kuwawezesha kuvuna zao hilo bila ya usumbufu wa aina yeyote na kwa muda muafaka.

Aidha amesema kuwa wamejipanga kuwasajili wote wanaokodi mashamba ya serikali na ya watu binafsi  ili kuhakikisha karafuu zote zinaenda kuuzwa ZSTC na sio pahala pemgine popote.

Dr. Said amefahamisha kuwa shirika linatarajia kukiboresha zaidi kitengo cha ulinzi ili kuona hakuna hata tembe moja ya karafuu inayosafirishwa kimagendo.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wote kuuza karafuu zao ZSTC ili kuisaidia serikali kupata mapato na kuiwezesha kutoa huduma kwa jamii ambazo ni muhimu.

Katika ziara hiyo Dr. Saidi alibahatika kutembelea maeneo ya Mahudusi,Kichunjuu, Mtambile, Mgelema,pamoja na Makuwe katika shamba la Serikali na kujionea jinsi karafuu zilivozaliwa kwa wingi ambapo ni tofauti na miaka 10 iliyopita.