JUMLA ya vipolo 18 vyenye karafuu kavu na magunia matatu makonyo, yamekamatwa na askari wa operesheni ya kuzuia magendo, inayoendeshwa na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zikiwa tayari kusafirishwa magendo wilaya ya Micheweni.

Akizungumza  kwa niaba ya mkuu wa operesheni hiyo Luteni Kanali Jabir Hamza, alisema karafuu hizo zimekamatwa Shehia ya Tondooni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati askari wakiwa katika doria za kawaida.

Luteni Jabir alieleza kuwa Septemba 3, mwaka huu majira ya 10:00 alfajiri katika ufukwe wa bandari ya Tondooni wilayani humo, askari hao walizikamata karafuu pamoja na makonyo hayo zikiwa zinasubiri maji ya yajae ili ziweze kusafirishwa.

“Alfajiri ya leo (juzi), hapa Tondooni Wilaya ya Micheweni, vijana wetu wakiwa katika doria wamefanikiwa kuzima jaribio la kutaka kusafirisha karafuu hizo kwenda nje nchi, na operesheni hii itakuwa ni endelevu”, alifahamisha Luteni Jabir

Kwa upande wake Kamanda wa KMKM Komandi ya Pemba Khamis Taji Khamis ameeleza kuwa kikosi chake kitazianika na kuzitenganisha karafuu kavu na makonyo na baadae kuzipeleka Shirika la Biahara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) kwa ajili ya kuuzwa.

“Kwa sasa karafuu pamoja na makonyo hayo yapo chini ya KMKM wilaya ya Wete na baada ya kukauka zitakanikwa uongozi wa  ZSTC kwahatua zaidi”,alifafanua kamanda Taji.

Nae Kamanda wa Operesheni wa kikosi cha KMKM Pemba Hussein Mohamed Seif, amesema kuwa wafanyabiashara wa magendo wamekuwa wakiikosesha serikali mapato muhimu kwa ajili huduma za kijamii na maendeleo.

 Amewataka wafanyabiashara hao kuacha kuichafua sifa ya karafuu ya Zanzibar kwa kuzichanganya na makonyo pindi wanapoenda kuziuzaili kulinda hadhi ya karafuu ya Zanzibar  katika masoko ya nje.

Mbali na kukamatwa kwa karafuu hizo hakuna mtu au chombo kinachohusishwa na karafuu hizo.

Kufuatia kukamatwa kwa karafuu hizo jamii imetakiwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitawezesha kukamatwa kwa wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu uchumi kwa kusafirisha karafuu nje ya nchi.

Na: Hassan Khamis, Pemba