Rais Uhuru Kenyatta amefurahia ziara yake nchini Tanzania akiitaja kuwa yenye mafanikio kwa nchi zote mbili.

Kiongozi huyo aliyasema hayo mjini Nairobi baada ya kuwasili akitokea mjini Chato, mkoani Geita nchini Tanzania anakotoka Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Katika mapokezi yake yaliyohudhuriwa na Naibu wake William Ruto na Gavana wa Jiji la Nairobi, Mike Sonko, Rais Kenyatta alieleza furaha yake kujumuika na Watanzania na kumshukuru Rais Magufuli kwa mwaliko wake. Amesema dhamira ya ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kijirani baina ya Kenya na Tanzania ulioanzia tangu enzi za Baba wa Taifa hilo, Mzee Jomo Kenyatta na mwenzake wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema viongozi wa kwanza wa mataifa hayo rafiki walikuwa kama pacha kutokana na kufanya kazi kwa uelewano mkubwa na kuwataka viongozi wa sasa wa mataifa hayo akiwamo yeye mwenyewe kuiga mfano huo na kuzifanya nchi hizo kuendelea kuwa pacha.

Rais Kenyatta alieleza umuhimu wa viongozi kuwajibika kuhakikisha vikwazo vinavyozuia kufanya biashara vinaondolewa, kuruhusu mzunguko huru wa watu na kuzidi kuimarisha uhusiano na kusisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika Mashariki kushikana kama kitu kimoja.

Chanzo Habari leo.