Kesi ya aliyekua mbunge wa Singida Mashariki na mnadhimu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu inatajwa leo katika Mahakama Kuu nchini Tanzania. Kesi hiyo ni ya kupinga uamuzi wa kuvuliwa kwake ubunge kutokana na kutohudhuria vikao vya bunge kwa karibu miaka miaka miwili.

Lissu amefungua kesi mahakamani chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka kisheria kufanya hivyo

Mwandishi wa BBC, Asha Juma amezungumza na Tundu Lissu akiwa nchini Ubelgiji kuhusu uwepo wake mahakamani, ambaye amesema

”Kesi inapopangiwa siku ya kusikilizwa au kutajwa au kwa hatua nyingine za kimahakama, pande zote huitwa mahakamani ni nyinyi mnaovutana au wawakilishi wenu wa kisheria au mawakili wenu”.

”Mimi nimefungua kesi kwa kutumia mwakilishi wa kisheria, mtu ambaye nimempa mamlaka kwa maandishi ili kufungua kesi yangu na kuiendesha kwa niaba yangu”.

Akizungumzia kuhusu yeye kutofika mahakamani pamoja na kutakiwa kufika mahakamani bila kukosa na pia kuwasilisha vielelezo vyote atakavyovitumia kwenye kesi hiyo Lissu alisema:

Anayetakiwa kufika mahakamani ni mtu mwenye mamlaka ya kisheria aliyompatia yeye Lissu mwenyewe.

Kuhusu shutuma dhidi yake kuwa alikuwa hajahudhuria vikao vya bunge bila taarifa Lissu amesema kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017.

Lissu amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu mbunge anayeumwa sio wajibu wa mbunge mwenyewe, ni wajibu wa waganga walioajiriwa na bunge.