Kesi inayomkabili mshitakiwa Iddi Ali Iddi,25, mkaazi wa Fundo Kimeleani, alietenda kosa la kuua, imeahirishwa katika mahakama ya mkoa Chake Chake, kutokana na kutokuwepo kwa hakimu husika.

Mara baada ya mshitakiwa huyo kutinga kizimbani akisubiri taratibu za mahakama, ndipo wakili wa serikali kutoka Ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka, Juma Ali Jumam alipodai shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikilizwa lakini hakimu anaeshughulikia kesi hiyo hayupo.

“Mheshimiwa hakimu shauri hili lipo kwa ajili ya kusikilizwa lakini hakimu husika hayupo, hivyo naiomba mahakama yako tukufu kuliakhirisha shauri hilo hadi tarehe nyengine,” alidai.

Hakimu wa mahakama hiyo, Luciano Makoye Nyengo, alikubaliana na ombi hilo na kusema kesi hiyo itarudi tena Juni 18 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa Agosti 7 mwaka 2018 baina ya saa 10:00 jioni na saa 12:00 jioni Fundo Kimeleani, ambapo alimuua Salma Simai Ali.

Kufanya hivyo ni kosa kisheria kinyume na kifungu cha 179 na kifungu cha 180 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.