Mwenyekiti wa Chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtangaza Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Aidha Profesa Lipumba amemtangaza mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya kuwa naibu katibu mkuu Bara na Fakhi Suleiman Khatibu kuwa naibu katibu mkuu Zanzibar.

Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando anachukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad.

Katibu mkuu huyo mpya, amepatikana baada ya kuchaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi lililokutana jana Ijumaa.

Hata hivyo, hatima ya viongozi hao wapya wa CUF akiwamo Profesa Lipumba aliyechaguliwa na mkutano mkuu Jumatano iliyopita Machi 14, 2019, itajulikana baada ya hukumu itakayotolewa Jumatatu ya Machi 18, 2019 na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Hukumu hiyo ni ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachana wa chama hicho upande wa Maalim Seif wakipinga uhalali wa Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF.