Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi mitatu ametelekezwa stendi kuu ya mabasi ya Ubungo jijini Dar es Salaa leo alfajiri Aprili 24.

Mtoto huyo amepelekwa ofisi za utawala za stendi ya Ubungo wanakoendelea kufanya matangazo ya kumtafuta mama yake huku wakimpatia huduma ya kwanza.

Abiria aliye telekezewa mtoto huyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, amesema asubuhi kuna mama alimuomba amshike mwanae akiaga anaenda chooni lakini hakurejea tena.

“Nilimsubiri kwa saa nzima hakuonekana ikabidi niende kutoa taarifa utawala na baadaye polisi,”  amesema abiria huyo aliyefika jana usiku akitokea mkoani Tabora.

Meneja wa kituo cha Ubungo, Imani Ernest amesema wanachosubiri ni mtoto huyo kuchukuliwa na polisi ili hatua za awali za kumpeleka ustawi wa jamii zifanywe.

“Mtoto tumempatia huduma ya kwanza kama maziwa na tunasubiri hatua zinazofuata,” amesema.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Ubungo, amesema wanampeleka mtoto huyo ofisi za ustawi wa jamii ili hatua nyingine ziendelee wakati wakimtafuta mama yake.