Mahakama ya Mwanzo ya Ipembe mjini Singida, imemhukumu mkazi wa mtaa wa Minga, Bahati Martin (39), kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutamka maneno ya kwamba atamuua Rais John Magufuli.

Mshtakiwa anadaiwa kuropoka maneno hayo Novemba 26, mwaka huu, huku siku ya pili yake (Novemba 27) Rais Magufuli na msafara wake ukipita mkoani Singida kwa njia ya barabara kwenda Chato.

Hakimu wa Mahakama hiyo, Yohana Zakaria, alitoa adhabu hiyo juzi baada ya kusema mahakama imetibitisha pasi na chembe ya shaka kwamba mtuhumiwa alitishia kwa maneno hayo, kosa ambalo ni kinyume cha kifungu cha 89 (2) (9) sura ya 16 ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Zakaria alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo katika eneo la kituo kikuu cha mabasi cha zamani mjini Singida, kwenye meza maarufu ya kuuzia magazeti, inayosimamiwa na kijana aliyetajwa kwa jina la John.

Alisema baada ya mshtakiwa kuropoka maneno hayo, mara moja raia wema waliripoti katika kituo kikuu cha polisi askari wa jeshi hilo walifika na kumtia mbaroni.

Kijana huyo aliyefungwa awali alikuwa akijihushisha na kazi ya kuonyesha picha, hususan mipira kupitia kibanda stendi hapo.

Hakimu Zakaria alisema baada ya kukamatwa na polisi, alikiri kutamka maneno hayo na hata alipopandishwa kizibani pia alikiri kosa lake.

Pamoja na kukiri huko, lakini alijitetea kwamba alifanya hivyo akiwa na lengo la kutania tu wala hakuwa na lengo la kuua.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Hakimu Zakaria alisema Rais wa nchi ni nembo ya taifa, hivyo mtu anapotishia uhai wake ni sawa na kutishia amani na usalama wa nchi kwa ujumla, hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa alilofanya.

“Mshtakiwa pamoja na kuwa hujaisumbua mahakama hii inakupa adhabu ya kutumikia jela miezi 24 ili iwe fundisho kwako na wengine wanaokusudia kufanya kosa kama hili. Adhabu hii iwaogopeshe wengine wanaotarajia kufanya makosa ya aina hii,” alisema hakimu.

Baada ya hukumu hiyo, mshtakiwa alipelekwa jela kuanza maisha mapya ya kutumikia kifungo chake cha miaka miwili.