Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ,Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe amezitaka jumuiya za gari za abiria kufuata  utaratibu  uliowekwa na Wizara ya Afya kwa lengo la  kuepuka  maambukizo ya maradhi ya corona.

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Bodi ya  Usafiri  Barabarani Mwanakwerekwe katika kikao cha Idara ya Leseni na jumuiya za gari za abiria kwa Mikoa mitatu ya Unguja.

Amesema ni vyema kwa madereva na makonda kufuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya afya ili kudhibiti kuenea kwa janga la maradhi ya corona.

 “Ni vyema kufuata masharti yaliowekwa na wataalamu kwani maradhi hayo si ya kuyafanyia mzaha hata kidogo”.amesema katibuhuyo.

Aidha amewataka viongozi wa jumuiya kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa  vyombo vya usafiri kwa abiria wanaotumia usafiri wa nchi kavu ili kudhibiti kuenea kwa maradhi ya corona.

Nae Kamishna Msaidizi wa Polisi  ambae pia ni  Mkuu wa Trafik Zanzibar Robert Hussein amewataka madereva na makonda wa gari za abiria kufuata maelekezo yanayotolewa na jeshi la polisi  kwani kwenda kinyume ni kosa  kisheria.

Na Kijakazi Abdalla – Maelezo