Kiongozi huyo amesema kuwa, ili kuendelea mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini, Washington, inatakiwa kwanza ibadili siasa zake kuihusu nchi hiyo. Kim Jong-un ameongeza kwamba kushindwa mazungumzo na Marekani, kuna maana ya kuongezeka mizozo katika eneo la Rasi ya Korea.

Amesema kuwa, hatopendelea kukutana na Rais Donald Trump wa Marekani, iwapo rais huyo hatofuata mwelekeo sahihi. Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini pia ameipa Marekani muda wa hadi mwishoni mwa mwaka huu (2019), iwe imechukua hatua madhubuti kwa ajili ya kubadilisha mazingira ya sasa sambamba na kufuata mwelekeo mpya kuihusu Pyongyang.

Onyo la Kim Jong-un kwa Marekani juu ya udharura wa kubadilishwa siasa za nchi hiyo kuihusu Pyongyang, imetolewa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kusisitiza kwenye kikao chake na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini kwamba ataendelea kuiwekea vikwazo serikali ya Pyongyang.

Trump ametangaza msimamo huo, katika hali ambayo, Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini alikuwa amefanya safari nchini Marekani kwa ajili ya kumshawishi rais huyo wa Marekani kuiondolea Pyongyang baadhi ya vikwazo, suala ambalo hata hivyo halikufikiwa katika safari yake hiyo.

Kuendelea kwa misimamo ya uhasama ya Trump dhidi ya nchi hiyo ya Asia, kunajiri katika hali ambayo ilitazamiwa kuwa baada ya Washington na Pyongyang kukubaliana kuendelea na mazungumzo yao, White House ingeiondolea baadhi ya vikwazo Korea Kaskazini kwa ajili ya kuleta hali ya kuaminiana na kuyafanya mazungumzo hayo yaweze kupiga hatua zaidi mbele.