Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un na Rais wa Urusi Vladimir Putin wameahidi kuboresha mahusiano katika mkutano wao wa kwanza kuwahi kufanyika.

Wawili hao walisalimiana kwa mikono katika kisiwa cha Russky karibu na mji wa bandari wa Vladivostok, mashariki mwa Urusi.

Ikulu ya Rais wa Urusi ya Kremlin imesema kuwa watajadili mpango wa kuacha matumizi ya nyuklia lakini bwana Kim inasemekana pia yuko huko kuomba msaada baada ya mazungumzo na Marekani kutozaa matunda.

Rais wa Marekani Donald Trump na Bwana Kim walikutana Hanoi mapema mwaka huu lakini wakashindwa kufikia mapatano yoyote.

Kiongozi wa Korea Kaskazini alikaribishwa kwa upendo na maafisa wa Urusi alipowasili Jumatano.