Idara ya ujasusi ya Afghanistan imesema vikosi maalum vya Afghanistan vimemuua kiongozi muhimu wa kundi la Al-Qaeda, Abu Muhsin al-Masri ambaye pia alikuwa akitafutwa na Marekani.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Kitaifa ya Usalama nchini Afghanistan, imeeleza kuwa Mmisri huyo aliyechukuliwa kama kiongozi namba mbili wa kundi la Al-Qaeda na mwenye ushawishi zaidi kwenye kundi hilo katika kanda hiyo ya India, aliuawa katika mkoa wa Ghazni katikati mwa Afghanistan.

Al-Masri alikuwa ameshitakiwa nchini Marekani kwa kutoa ufadhili wa bidhaa na rasilimali kwa shirika moja la kigeni linalohusika na ugaidi na pia, kwa njama ya kuwauwa raia wa Marekani.