Wakati wowote Kocha Maurizio Sarri anaweza kutupiwa virago Chelsea, baada ya jana kupata matokeo mabaya zaidi katika Ligi Kuu England.

Kitendo cha Chelsea kufungwa mabao 6-0 na Manchester City kinamuweka pabaya Sarri ambaye tangu alipotua Chelsea ameshindwa kupata mafanikio.

Timu hiyo ilicheza chini ya kiwango baada ya kufungwa mabao manne ndani ya dakika 25 za kipindi cha kwanza.

Hii ni mara ya kwanza Chelsea kupata matokeo mabaya baada ya miaka 27 tangu klabu hiyo yenye maskani Stamford Bridge ilipoanzishwa.

Guardiola alisema Sarri ni kocha bora na alipenda kuona mechi za Napoli alipokuwa akiinoa kabla ya kujiunga na Chelsea kumrithi Mtaliano mwenzake Antonio Conte.

Katika hatua nyingine, Sarri aligoma kumpa mkono Guardiola, baada ya mchezo kumalizika.

Baada ya mchezo Guardiola alimfuata Sarri kumpa mkono, lakini kocha huyo aligoma kutoa mkono.

Badala yake Guardiola alizungumza kwa muda mfupi na kocha msaidizi Gianfranco Zola.