Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi asema kuwa  udanganyifu wa Mitihani ya Taifa ya Darasa la 10 { Form 11} uliotokea na kulazimisha Serikali kufuta Mitihani yote haukubaliki hata kidogo kwa vile una nia ya kutaka kuliangamiza Taifa Kimaendeleo.

Alisema hakuna Serikali hata moja Duniani inayokubali kuchezewa Elimu yake na uamuzi aliochukuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wa kufuta mara moja Mtihani wote wa Darasa la 10 baada ya kugundua kuvuja kwa Mitihani ni uthibitisho  kwamba Serikali kamwe haitokubali kutokea upuuzi huo

Akitoa Hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Baraza la 9 la Wawakilishi  huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukuwa hatua kali na za Kisheria dhidi ya wale wote waliohusika na uhalifu huo wa kuvuja kwa Mitihani.

Balozi Seif aliviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wahusika wote walioshiriki  kwenye  uhalifu huo na wanatakaobainika  na hujuma hizowapelekwe Mahakamani mara moja kujibu dhambi zinazowakabili.

“ Tutang’oa Miti hata kama ni mikubwa kama Mbuyu, Miche, Mizizi na mbegu zinazosubiri kuchipua ili tukio hili lililoitia  aibu Serikali yetu lisitokezee tena”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wote  wa Zanzibar washirikiane na Serikali katika kupiga vita uhalifu kama huo ambao ukiachiliwa utaliangamiza Taifa huku akiiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuchukuwa tahadhari zote ili udanganyifu wa Mitihani Nchini usitokee tena.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

06/12/2018.