Mfanyabiashara mkazi wa Nairobi nchini Kenya, Abshir Hachi Afrah (56), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka matatu yakiwamo kukwepa kodi, kuisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kutakatisha Sh. bilioni 8.107.

Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni raia wa Somalia, alisomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Janeth Mtega.

Simon alidai kuwa kati ya 2015 na 2018 jijini Dar es Salaam, mfanyabiashara huyo alikwepa kulipa kodi wakati wa kusambaza ya mafuta ya petroli.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na tarehe za tukio la kwanza, katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam, kwa kitendo chake cha ukwepaji wa kodi aliisababishia hasara mamlaka hiyo Sh. 8, 107,509,385.48 kinyume cha Sheria ya Kodi ya mwaka 2015.

Katika mashtaka ya tatu, ilidaiwa kuwa mshtakiwa alijipatia Sh. bilioni 8.107 kwa kukwepa kulipa kodi wakati akijua kwamba fedha hizo ni zao la uhalifu ambalo ni la kutakatisha fedha.

Hakimu Mtega alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo kuomba  mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mtega alisema kesi hiyo itatajwa Juni 4, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kwa sababu mashtaka hayo hayana dhamana