Kocha Simba akataa nyumba ajiweka hotelini

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, ameuambia uongozi wa timu hiyo kuwa, anataka kuendelea kukaa hotelini kwa kuwa amezoea na pia hajui kupika.

Aussems jana Jumamosi aliiongoza timu hiyo kucheza dhidi ya Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa tatu kwake na wa kwanza wa ugenini katika ligi ya msimu huu ambao ulienda suluhu ya kutokufungana.

Ikumbukwe, Mbelgiji huyo alifikia katika Hoteli ya Golden Tulip ya Masaki kabla ya kuhamishiwa katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach mara baada ya kuanza kazi kwenye timu hiyo na japo hulipa chumba Sh 170,000 kwa siku.

Kwa mujibu wa gazeti la Championi Jumamosi, Aussems alisema hawezi kukubali kuishi kwenye nyumba za kupangiwa kwa kuwa maisha yake ya ukocha amekuwa akiishi hotelini.

“Kwa hapa ndiyo sehemu ambayo nitaendelea kuishi kwa muda wote, nilishawaambia viongozi na hilo wanalijua hivyo siwezi kwenda kuishi kwenye nyumba yoyote zaidi ya hapa.

“Unajua kwanza sijui kupika halafu maisha ya hotelini nimeyazoea tangu nimeanza kufanya kazi Afrika nimekuwa nikiishi hoteli sawa na hapa na uzuri huwa sichagui chakula ili mradi kiwe kitamu,” alisema Aussems.