Kocha mkuu wa klabu ya JKU Ramadhan Issa Pele ametoa siri ya mafanikio ya klabu yao kuchukua Ubingwa wa ligi kuu ya Zanzibar msimu wa mwaka 2017/2018 ni mashirikiano baina ya viongozi na wachezaji kila hatua ya ligi kuu ya Zanzibar.

Aidha Ramadhan Pele amesema hatua hiyo ni kubwa sana kwa maendeleo ya klabu ya Jku kwa mipango ya muda mrefu ambayo walikuwa nayo kwenye kukuza timu yao .

Kwa upande mwengine Ramadhan Pele amesema licha ya kukabiliana na mashindano makubwa ya kimataifa mbele yao sasa umefika wakati wa kubadilika kwa timu yao kutengeneza kikosi bora zaidi.

Kuhusu udhamini wa ligi kuu ya Zanzibar Pele amesema Jku moja ya vilabu vinavyokumbwa na matatizo ya kifedha licha ya kuonekana klabu bora kwa Zanzibar kwa kiwango cha mpira lakini bado fedha ni changamoto kwao na kuwataka viongozi wa ZFA kuhakikisha suala hili linatafutiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake nohodha wa klabu ya Jku Posiana Malik amesema wamefarijika sana kwa kuandika rekodi hiyo kubwa kwenye soka la Zanzibar ambayo ilishikiliwa na KMKM.

Aidha amesema ubingwa huo unaifanya Jku kuwa juu kimataifa na kushiriki mashindano mengi ya kimataifa kama vile ya Kagame Cup na kuitangaza klabu yao.

‘’ Tunashukuru sana mwaka huu ligi imekuwa ngumu sana tumepishana na Zimamoto kidogo tu sasa tunajipanga kwenye usajili ili kutafuta timu ya kushindana kimataifa’’ Alisema Posiana Malik.

JKU wamechukua ubingwa wa ligi kuu ya Zanzibar wakiwa na alama 33 dhidi ya Zimamoto wenye alama 32 Jku wanatarajia kupewa zawadi zao kwenye mchezo wa ngao ya hisani tarehe 18 mwezi wa Oktoba.