Kushuka Sh. bilioni saba hadi nne ya mapato ya mpasua kichwa Meya

Kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kutoka Sh. bilioni saba hadi nne kuna ‘mpasua kichwa’ Meya wa Manispaa hiyo, Raymond Mboya.

Mapato hayo yameshuka kutokana na kubadilishwa kwa mfumo wa ukusanyaji kodi ambazo serikali kuu imezichukua na kuhamishia jukumu la ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo kama kodi za ardhi, majengo na matangazo katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akizungumza katika jukwaa la elimu ya mlipa kodi kwa watumishi wa manispaa hiyo ambalo liliandaliwa na TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Mboya ameeleza namna yeye na wenzake katika Baraza la Madiwani wanavyofikiria vyanzo vipya vitakavyoinyanyua kimapato halmashauri hiyo.

“Hiyo tofauti ya Sh. bilioni tatu inatokana na vyanzo tulivyokuwa tukivitegemea kama halmashauri, kodi yake kukusanywa na TRA

“Kwa sasa Manispaa ya Moshi imebuni vyanzo vipya vya mapato na imeweka mkazo wa ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vilivyobaki kama kwenye urejeshwaji wa baadhi ya vitega uchumi ambavyo vilikuwa chini ya mwekezaji baada ya muda wake kuisha. Halmashauri itavisimamia yenyewe ili kufikia malengo ya bajeti ya maendeleo.”Mboya alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wao wa kukutana na watumishi wa manispaa pamoja na madiwani, Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, alisema mamlaka hiyo imewakutanisha pamoja ili kueleweshana maeneo na mipaka ya ukusanyaji wa mapato kati ya serikali za mitaa na serikali kuu.

“TRA tuliona ni vyema kukaa pamoja na watumishi wa manispaa na madiwani husika na kueleweshana kuhusu ukusanyaji wa kodi, pasipo kuathiri vyanzo vya mapato vya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi,” ameeleza Mbibo

Ameeleza Mbibo ambaye hivi karibuni Rais John Magufuli alimmwagia sifa kwa kukataa rushwa ya Dola za Marekani 2,000 kutoka kwa mtu aliyetaka apewe nafuu ya kodi anayodaiwa.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mawenzi, Aloyce Silayo, amesema changamoto kubwa inayojitokeza kwa sasa ni kukosekana kwa elimu ya ulipaji wa kodi kwa watumishi wa serikali na wananchi.