Sheria ya Kiislamu, (Sharia) mara nyingi huhusishwa na wakosoaji kwa kuwa na adhabu na misimamo mikali. Lakini mwanamke mmoja ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Sharia nchini Malaysia anasema cheo chake kinampa nafasi ya kuwalinda wanawake katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi.

Jaji Nenney Shushaidah husikiliza zaidi ya kesi tano kwa siku, na kwa wiki huweza kusikiliza mpaka kesi 80.

Nchi ya Malaysia inafuata mrengo wa kati wa Uislamu lakini misimamo ya kihafidhina imekuwa ikikuwa na kuchochea matumizi zaidi ya Sharia. Nchi hiyo inatumia mifumo miwili ya kisheria, maelfu ya Waislamu hutumia Sharia kwenye migogoro ya kiimani na kifamilia. Ambao si waisilamu hutumia sheria za kawaida katika kutatua migogoro yao kama hiyo.

Jaji Shushaidah hutoa hukumu kwenye kila kitu kuanzia kesi za kifedha mpaka kwenye kesi za Khalwat (kesi za watu wasiooana wanaokutwa katika mazingira ya kutatanisha).

Weledi wake hasa upo katika eneo la malezi ya watoto na kesi za ndoa za mitara – Sharia inaruhusu mwanaume wa kiislamu kuoa mpaka wake wanne.

Kwa mujibu wa jaji Shushaidah kuna vitu vingi vya kutazamwa kabla ya kuruhusu ndoa ya mitara.

“Kila kesi ina upekee wake,” amesema. “Hauwezi ukalinganisha kila kitu na kusema sheria ya kiislamu inawapendelea wanaume na kuwakandamiza wanawake… Nataka kurekebisha hii dhana potofu.”

Nenney Shushaidah adjusts her robesJoho langu linanikumbusha uzito wa kazi yangu kama jaji wa Sharia’

Pande zote ambazo zitakuwemo kwenye ndoa ya mitara wanatakiwa kufika wenyewe kwenye kesi itakayosikilizwa na Jaji Shushaidah.

“Nataka kusikia kutoka kwa kila mmoja wao, na si mwanaume pekee,” amesema. “Naongea na wanawake ili kujua kama wote wanakubaliana na mpangilio huo. Ni muhimu wakubali maana nikiona dalili yeyote ya kutokukubaliana sitotoa kibali cha ndoa ya mitara.”

“Mimi ni mwanamke na ninafahamu kuwa wanawake wengi wasingependa jambo hilo (mitara). Lakini imeruhusiwa katika Uislamu, na mahakama zetu hapa Malaysia zimetunga sheria kali za kuliongoza jambo hilo.”

“Mwanaume inampasa awe na sababu ya msingi sana ili aongeze mke mwengine,” amesema.

“Lazima aoneshe kuwa ana uwezo wa kutunza maslahi ya mke wa kwanza na ya wanawake wengine atakaooa. Haruhusiwi kupuuzia mahitaji ya mke yeyote.”

Jaji Shushaidah amedai wapo baadhi ya wake wanoounga mkono waume zao kuongeza wenza.

Anakumbushia kesi moja ya mwanamke ambaye alikuwa na maradhi makali na asingeweza kupata watoto.

“Alikuwa akimpenda sana mumewe na kataka nimpe ruhusa ya kuongeza mke wa pili. Nilitoa kibali.

Jaji huyo anatetea sifa ya dini yake ya kuwa na sheria kali kwa kusema inaleta usawa pia.

Lakini wakosoaji wanasema mara nyingi Sharia inatumiwa vibaya na kusema “Dini sio kisingizio kinachokubalika cha kuvunja sheria za kimataifa za haki za binaadamu na usawa.”

Makundi ya wakosoaji yamelaani hukumu ya hivi karibuni ya kuwachapa viboko wanawake wawili ambao ni wapenzi waliokamatwa kwa kosa la kujaribu kufanya mapenzi.

Jaji Shushaidah hakutaka kuzungumzia kesi hiyo na kudai: “Viboka katika Sharia ni adhabu ambayo inawakumbusha wakosaji kutorudia makosa yao.”

Pia anasema si kweli kwamba mfumo huo unapendelea tu wanaume.

“Sheria zetu zipo ili kulinda haki za wanawake. Zinaangalia maisha yao na maslahi yao kwa ujumla,”amesema.

“Uislamu unawaweka wanawake katika mizani ya juu na kama majaji inatupasa kurudi katika misingi na kudumisha hilo kwa kupitia Sharia.”

Mashaka yake makubwa yapo kwa wanaume wa nchi hiyo ambao wanakwepa mahakama za nch hiyo kwa kwenda nje ya nchi kuongeza wake.

“Hawezi kubanwa na mfumo wetu kama ataenda kuoa nje ya nchi. Baadhi ya wanawake wanaunga mkono hilo lakini hawajui ni kwa namna gani inawaumiza. Sheria zetu zinawatetea kwa kuwafanya wanaume kuhusika kwa kila wafanyalo.”

Makundi kama Sisters in Islam wamekuwa wakikosoa mfumo wa nchi hiyo wakidai mahakama za Sharia zina uwakilishi mdogo wa wanawake na zimekuwa zikielemea kwenye mfumo dume.

“Mfumo mzima wa Sharia hapa Malaysia unawabagua wanawake, inawafanya waonekane ni chanzo cha matatizo ya kimaadili kwenye jamii,” amesema Majidah Hashim ambaye ni msemaji wa kundi hilo.

Nenney Shushaidah

Kutokana na upungufu huo, uteuzi wa Jaji Shushaidah kuwa jaji wa kwanza wa mahakama hizo unachukuliwa kwa uzito mkubwa.

“Siku za nyuma, majaji wengi wa mahakama za Sharia walikuwa wanaume na walikuwa wakipinga wanawake kushika nyadhifa hizo,” amesema Jaji Shushaidah.

“Sikuwahi kuota kuwa Jaji” amesema. “Nikiwa mwanasheria. Sikuamini kuwa ningeweza kufanya kazi kubwa ya kushughulikia kesi nzito. Na kama mwanamke niliogopa na kutojiamini.”

“Wakati mwengine huwa ninajisikia uzito. Kama mwanamke lazima nijisikie hivyo, na nitakuwa muongo kama nitasema vinginevyo. Lakini mimi ni Jaji inabidi na yanipasa kuwa muwazi na kuepuka upendeleo. Hivyo katika maamuzi yangu, najitahidi kutilia maanani mambo hayo.”

Chanzo: BBC