Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu  alipata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali mbunge mwenzake kutoka mkoa huo, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Tundu Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki amelazwa hospitalini hapo akitibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiofahamika akiwa bungeni mjini Dodoma.

Akiwa hospitalini hapo, Nyalandu amesema kuwa hali ya mbunge huyo inaonyesha kuwa alishambuliwa vibaya sana na kwamba kazi kubwa ya madaktari wanayofanya kwa sasa ni kuhakikisha mwili wake unaimarika ili aweze kupata matibabu zaidi yanayostahili.

“Nimeonana na Mh. Tundu lissu katika chumba chake hospitali ya Nairobi na kuzungumza naye kuhusu hali yake na anavyoendelea. Ukweli ni kwamba, ameumizwa vibaya. Imeelezwa kwamba Madaktari wanaendelea na hatua kadhaa za matibabu, wakiwa wameanza kwa kumuimarisha (stabilization), ili kuufanya mwili uweze kumudu hatua zaidi za utibabu anazopaswa kufanyiwa.”

Katika mazungumzo yake na Tundu Lissu, Nyalandu amesema kwamba Lissu alifurahishwa na ujio wake na kwamba alimshukuru Mungu kwa kuzidi kumuweka hai licha ya tukio hilo la kutisha lililomtokea.

“Katika kuongea naye, Mh. Lissu ameonesha uso wa tabasamu, huku akimshukuru Mungu kwa kumruhusu kuwepo hai.”

Naamini kwamba hatua zaidi na za haraka zitahitajika kumsaidia apate huduma za kitabibu katika ubora na ufanisi uliopo kwa sasa duniani, alisema Nyalandu.

Aidha, aliendelea kusisitiza kwamba, ni maombi yake kwa watanzania, waweke pembeni tofauti za kiitikadi, ama mitazamo, waungane na kushikamana kama Taifa kwa ajili ya kumwomba Mungu anyooshe mkono wake, na kumponya Tundu Lissu.

Nyalandu pia amewasisitiza watanzania kutoa chochote kile walichonacho kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Tundu Lissu aweze kupona na kurejea kulitumikia taifa.