Katika mechi ya kufa kupona timu ya Tanzania Taifa Stars inakutana ana kwa ana leo na Harambee stars ya Kenya uwanjani kwenye michuano ya kombe la mataifa ya Afrika kutafuta pointi tatu muhimu.

Kuna Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars ya Kenya.

Hayo ni majina ya timu hizo ambazo zinapambana leo kwenye mechi ya Afcon ambayo ndiyo gumzo kuu leo nchini Kenya na Tanzania, na kwa jumla Afrika Mashariki.

Tanzania na Kenya zilianza na mkosi mashindano ya Afcon 2019.Tanzania iliangukia pua mechi yao kwanza kwa kushindwa na Senegal mabao 2-0 kisha Kenya nao wakaadhibiwa kwa mabao hayo hayo na Algeria.

Wadadisi wanasema Kenya ina nafasi kubwa ya kupata pointi tatu wakizingatia takwimu za mechi kati ya mataifa haya mawili.Kwanini?

Kufikia sasa timu hizo mbili zimekutana mara tisa, na Tanzania ikashinda mechi mbili tu.Macho yote yanaangazia Cairo sasa kuona jinsi Mbwana Samatta atakavyoongoza kikosi chake dhidi ya nahodha mwenzake wa Kenya Victor Wanyama.

Lakini ni wazi kwa timu zote mbili kwamba mechi ya leo ni kibarua kipevu.

Mchezaji wa Harambee Stars Michael Olunga ameeleza, ‘Tanzania ni jirani zetu na itakuwa mechi ngumu. Sote tulishindwa katika mechi zetu za ufunguzi. Kikombozi chetu sasa ni pointi tatu’.

‘Tumejifunza kutokana na makosa yetu na tutajisahihisha katika mechi ijayo’, ameongeza Olunga.

Taifa Stars wapo chini ya nyota MbwanaSamatta, ambaye kufikia sasa ameifungia timu ya taifa mabao 17.

Kenya inacheza katika mashndano hayo kwa mara ya kwanza tangu 2004 na wamefanikiwa kushinda mechi moja pekee katiya 15 zake za nyuma katika mashindano hayo lakini kocha Sebastien Migne amesema kwamba “hakuna lisilowezekana” iwapo timu yake itafaulu kuifunga Tanzania.

Wameorodheshwa juu ya jirani zake katika eneo la Afrika mashariki, huku Tanzania ikiwa imecheza mara moja tu katika mashindano hayo mnamo 1980.

View image on Twitter

Waswahili wanakwambia mtoto hatumwi dukani leo!

Mitandao nayo hayashikiki kutokana na cheche za raia wa mataifa hayo wakijitosa kuonyesha ushabiki wao kwa timu hizo mbili za Afrika mashariki

Kocha raia wa Nigeria Emmanuel Amuneke ameleta matumaini kwa Tanzania baada ya kuisukuma timu hiyo kufuzu katika mashindnao hayo nchini Misri.

Hii ikiwa ni mara ya kwanza kufuzu tangu 1980.

View image on Twitter

Matarajio sasa na swali kubwa ni je Taifa Stars italitingisa eneo la Afrika mashariki baada ya kurudi katika michuano hiyo?.

Msisimko ni mkubwa kwa mashabiki wa kambi zote mbili, msema kweli akisubiriwa kujulikana.