Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amesema kuwa amemuandikia barua mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC kumtaarifu kuwa kiti cha Ubunge wa jimbo la Singida Mashariki kipo wazi, kutokana na Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Tundu Lissu (CHADEMA) kutokutoa taarifa ya wapi alipo na kutokujaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Akitaja sababu kubwa mbili, Spika amesema ni kutotoa taarifa rasmi ya maendeleo yake, huku akionekana sehemu mbalimbali.

Sababu ya pili ni kushindwa kujaza fomu za maadili ya viongozi za Tume ya maadili, hivyo kupoteza sifa za kuwa Mbunge.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kupitia ukurasa wao wa Twitter wamesema wamesikia kauli ya Spika na watatoa tamko juu jambo hilo muda mfupi ujao.