Ubalozi wa Palestina nchini Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) utafanya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) siku ya Jumatano tarehe 7 Disemba, 2016 kuanzia saa 3.00 za asubuhi hadi saa 6.00 mchana katika Ukumbi mkubwa wa mikutano wa Jengo la Kompyuta, Kampasi ya Tunguu.

 

Kwa kawaida maadhimisho haya hufanywa duniani kote kila ifikapo tarehe 29 Novemba ya kila mwaka. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio Namba 32/40 B la tarehe 2 Disemba, 1977 na Azimio Namba 34/65 D la tarehe 12 Disemba, 1979 uliitangaza tarehe 29 Novemba ya kila mwaka kuwa ni siku ya Kimataifa ya mshikamano na Watu wa Palestina ili kutambua haki ya watu hao kuwa na taifa huru na lenye mamlaka kamili ya kujitawala.

 

Mgeni rasmi katika maadhimisho haya ni Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Viongozi wengine wa serikali na taasisi za kiraia pamoja na Mheshimiwa Bwana Hazem Shabat, Balozi wa Palestina nchini Tanzania watakuwepo katika maadhimisho haya ambapo pia Mheshimiwa Bwana Shabat hatimaye atatoa mhadhara utakaoambatana na masuali na majibu.