Aliekua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif ameteuliwa kuwa mshauri mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, huku wenzake aliohama nao wakipangiwa majuukumu mbalimbali ndani ya chama hicho.

Maalim Seif na wenzake walijitoa CUF Machi 2019 baada ya kushindwa kesi waliyofungua Mahakama Kuu wakipinga uongozi wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na mgogoro ulioanza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Juni 10, 2019 na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu, kufuatia kikao cha kamati kuu ya ACT Wazalendo kilichoketi Dar es Salaam jana Jumapili, imesema Maalim Seif mwenye kadi namba moja ya chama hicho, ameteuliwa kuwa mshauri mkuu wa chama.

Katika nafasi za kamati kuu ya chama hicho, wafuasi wa Maalim Seif wameingizwa akiwemo Fatma Fereji na Eddy Riyami, huku pia kukiwa na wajumbe wengine waliongezwa ambao ni Theopista Kumwenda na Mwajabu Dhahabu.

Katika nafasi za wenyeviti wa Kamati za Kitaifa, Nassor Marzurui ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Miradi, huku Salim Bimani akiteuliwa kuwa  Mwenyekiti wa Kamati ya Itikadi, Mawasiliano na Uenezi na Joram Bashange akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya kampeni na uchaguzi.

Wengine ni pamoja na Ismail Jussa aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya mikakati, usimamizi na ufuatiliaji, huku mbunge wa zamani wa viti maalum.

Mhonga Ruhwanya akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya oganaizesheni, mafunzo na wanachama.