Mabilionea wengine sita waliotekwa Afrika mwaka 2018

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji, maarufu kama Mo limeitikisa Tanzania, lakini si jipya kwa mwaka huu barani Afrika.

Mo ni tajiri mkubwa wa saba barani Afrika kutekwa tangia mwaka 2018 ulipoanza.

Matukio mengine ya namna hiyo yametokea nchini Afrika Kusini, Msumbiji na Nigeria.

1.Shiraz Gathoo – Afrika Kusini

Mfanyabiashara maarufu kutoka Afrika Kusini alitekwa mnamo 10 Machi mwaka huu. Watekaji wake walijifanya kuwa ni askari wa usalama barabarani na kuweka kizuizi bandia barabarani na kumteka.

Aliachiwa huru mwishoni mwa mwezi Agosti baada ya kukaa mateka kwa miezi sita. Haijafahamika aliachiwa namna gani lakini wadadisi wahahisi alitoa komboleo la pesa kwa watekaji.

2.Liyaqat Ali Parker – Afrika Kusini

Mwezi Julai, Liyaqat Ali Parker mfanyabiashara kutoka Afrika Kusini pia alitekwa jijini Capetown akiwa katika majengo ya ofisi yake na watu waliokuwa na bunduki.

Parker, 65, ni mwanzilishi wa kampuni ya Foodprop Group ambayo humiliki maduka ya jumla ya Foodworld nchini humo. Anamiliki mali nyingine nyingi nchini humo.

Mfanyabiashara huyo alitekwa 9 Julai baada ya kufuatiliwa kwa muda na watu watano waliotumia gari aina ya double-cabin.

Alizuiliwa kwa miezi miwili hadi aliporejea kwake nyumbani mnamo 17 Septemba.

Siku ya kutekwa kwake, wanaume watano wasiojulikana wanadaiwa kulifuata gari lake hadi kwenye maegesho ya biashara yake Fairway Close, N1 City chini ya jengo.

Washambuliaji waliokuwa na silaha mwanzo walimshambulia mlinzi na kumfungia chooni na pia kumpokonya simu yake.

Baadaye walimtwaa mfanyabiashara huyo na kumuingiza ndani ya gari lao kisha wakatoroka naye.

3.Babake John Obi Mikel – Nigeria

Baba wa mchezaji nyota wa Nigeria John Mikel Obi pia alitekwa mwezi Juni na watu waliokuwa na silaha katika eneo la Enugu.

Alikuwa ametekwa mnamo 26 Juni lakini akaokolewa na polisi mnamo 2 Julai baada ya makabiliano makali kati yao na waliokuwa wanamzuilia.

Inadaiwa waliomteka walikuwa wanataka kikombozi cha £21,000.

Ilikuwa ni baada ya watekaji kupiga simu wakiitisha pesa ndipo polisi walipofanikiwa kuwafuatilia na kufahamu walikokuwa. Waliwavamia na baada ya ufyatulianaji wa risasi wakakimbia na kuwaacha mateka msituni.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Chief Mikel Obi kutekwa.

Awali alitekwa mwaka 2011 na watekaji kudai kikombozi. Obi alifanikiwa kuokolewa na polisi lakini mtoto wake anadai aliteswa wakati alipokuwa kizuizini.

4.Andre Hanekom – Msumbiji

Raia wa Afrika Kusini anayefanya biashara nchini Msumbiji Andre Hanekom alitekwa katika jimbo la Cabo Delgado Agosti katika mji wa Palma akiwa kwenye maegesho ya hoteli ya Amarula.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa ameishi Msumbiji kwa miaka 26 anadaiwa kuandamwa na wanaume wanne wasiojulikana na kufyatuliwa risasi mara kadha. Alikimbilia hotelini lakini akakamatwa na kuingizwa kwenye gari, na kutoroshwa.

Sababu za kutekwa kwake bado zina utata.

Kuna taarifa zilizodai kwamba waliomteka walikuwa wanajeshi wa kupambana na ugaidi na kwamba alikuwa anahusishwa na ugaidi. Lakini mke wake Francis alikanusha kwamba mumewe amewahi kujihusisha na ugaidi.

Alipatikana katika hospitali moja Palma akiwa anapokea matibabu chini ya ulinzi wa jeshi.

 

5.Sikhumbozo Mjwara – Afrika Kusini

Sikhumbozo Mjwara, 41, mfanyabiashara kutoka jijini Durban Afrika Kusini pia alitekwa mwezi Agosti na mpaka sasa bado hajulikani alipo.

Watu watatu wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea.

Mfanyabiashara huyo alitekwa akiwa nje ya mahakama ya hakimu mjini Verulam baada ya kuhudhuria kikao cha kusikizwa kwa kesi inayohusisha mzozo wa kifedha.

Mjwara ana kampuni zinazohusika katika biashara ya madini na pia mighahawa.

6.Robert Mugabe wa Uganda

Mmoja wa wafanyabiashara maarufu kutoka wilaya ya Nakasongola Robert Mugabe alitekwa nyara mnamo Agosti na watu waliokuwa wamevalia mavazi ya jeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mugabe, 38, alitekwa alipokuwa anasafirisha samaki kutoka Kasese kwenda Ishasha katika wilaya Kanungu walipokuwa wanapitia mbuga ya taifa ya Malkia Elizabeth.

Aliachiliwa huru siku chache baadaye baada ya familia yake kudaiwa kulipa kikombozi cha $7,500 ingawa awali waliomteka walidai $20,000.

Chanzo: BBC