TIMU ya madaktari bingwa 18 wa maradhi tafauti wanaounda Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu Duniani (WAMY) yenye makao yake nchini Saudi Arabia, imewasili Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kisiwani Pemba.

Hii ni mara ya pili kwa madaktari hao kufika  visiwani humu, ambapo mwaka 2016 pia walikuwepo mwezi Oktoba na kufanya kazi ya kutibu na kutoa huduma mbalimbali za kiafya kisiwani Pemba kwa muda wa siku kumi.

Akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wataalamu hao iliyofanyika Oktoba 13, 2016  usiku katika hoteli ya Mizingani mjini Zanzibar, Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo amesema, kazi inayofanywa na madaktari hao bila ya malipo, ina ujira mkubwa kwa Mwenyezi Mungu.

Alinukuu moja kati ya hadithi za Mtume Muhammad (SAW), aliposema, iwapo mtu atatoa mwiba katika mwili wa kiumbe mwenzake, hisani na fadhila zake hazifutiki na hubakia milele.

“Kwa kazi yenu nzuri ambapo mwaka jana mliwatibu wananchi wengi waliokuwa wanasumbuliwa na maradhi mbalimbali, sio tu mmetoa mwiba miilini mwao, bali mmewaponya ndwele zao na kuwarejeshea matumaini kiafya,” alifafanua.

Alieleza kufurahishwa kwake kwa kazi nzuri waliyofanya kuwatibu wananchi kwa aina mbalimbali za matibabu ikiwemo yaliyohitaji upasuaji pamoja na maradhi ya akinamama.

Waziri huyo alisema, kwa mujibu wa taarifa anazopata kutoka kwa wasaidizi wake, timu zote zilizowahi kuja Zanzibar kutoa huduma za afya zimekuwa zikifanya kazi nzuri, lakini jopo hilo ndilo lililofanya vizuri zaidi na kuleta matokeo bora.

“Kwa hakika mmefanya kazi nzuri na mnastahili pongezi, wananchi wetu wamezipenda huduma zenu, hivyo ninaamini mnaporudi tena mtafanya zaidi ya mwaka jana,” alisema Kombo.

Alifahamisha kuwa, mafanikio hayo ndiyo yaliyowafanya wananchi kisiwani Pemba wawamiminie sifa nyingi na tangu walipoondoka baada ya kumaliza shughuli iliyowaleta mwaka jana, wananchi hao wamekuwa wakitamani warudi tena.

Aidha aliwaambia madaktari hao kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeimarisha huduma za afya katika hospitali na vituo vyake kwa kuziongezea vifaa vya kisasa na wafanyakazi, hali aliyosema itarahisisha utendaji wa mabingwa hao.

Alisema huduma bora za afya ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye amekuwa na msaada mkubwa kwa Wizara ya Afya kuhakikisha mahitaji yote ya msingi yanapatikana kwa wakati ili kuimarisha sekta hiyo.

Aidha alisisitiza haja ya kukutana na madaktari hao mara wanapomaliza kazi ili kupata mrejesho na kutambua changamoto wanazokutana nazo ili serikali ijue namna ya kuzipatia ufumbuzi, badala ya utaratibu wa kuonana naye kabla hawajaingia kazini.

Waziri Kombo pia aliwaomba waratibu wa timu hiyo, kuhakikisha wanawapeleka madaktari hao katika hospitali ya Micheweni ambako kumekuwa na matatizo mbalimbali, ili kupata msaada wao wa kiushauri utakaoisaidia serikali kuitengenezea mazingira mazuri.

Mapema, kiongozi wa timu ya madaktari hao Profesa Sultan Said Baghdad, alisema wakiwa wanafanya kazi kisiwani Pemba, wanajisikia wako nyumbani kwa namna walivyooneshwa ukarimu na mahaba na wananchi wakati walipokuja mwaka jana.

Alieleza kufarijika kwake na jinsi wananchi wa Pemba walivyoonesha hamu ya kuwataka warudi tena, akisema hicho ni kielelezo cha kuridhwa na huduma za matibabu walizopata mara ya kwanza.

“Tukiwa tumeziacha familia zetu nyumbani, wakati tuko mbali na wapenzi na watu tuliowazoea, tukiwa nje ya mazingira tuliyozowea kufanya kazi, hatuoni tafauti yoyote hapa Zanzibar. Kwa kweli ni sawa na kuweko Saudi pamoja na familia na marafiki zetu,” alieleza Profesa Baghdad.

Kwa upande wake, Sheikh Abdalla Talib kutoka African Muslim Agency inayoratibu ziara ya madaktari hao, alisema hiyo ni fursa nzuri kwa wananchi wenye maradhi mbalimbali kisiwani Pemba kuonana na wataalamu hao kwa ajili ya kupatiwa tiba.

Aliwataka wananchi wenye matatizo ya kiafya ambayo wanahangaika nayo kwa muda mrefu bila ya mafanikio, wajitokeze kwa wingi kuonana na madaktari hao ili waweze kupata matibabu ya uhakika.

Sheikh Talib alisema timu hiyo itakuweko katika Pemba kuanzia leo Oktoba 14 hadi 24, mwaka huu.

Madaktari wa jumuiya hiyo ya WAMY ambao wanatoka nchi mbalimbali kama vile Saudi Arabia, Misri, Sudan na nyengine, wamebobea katika kutibu magonjwa tafauti ikiwemo ya mifupa, matatizo ya akinamama, pamoja na kufanya upasuaji kwa watu wenye matatizo ya mkono na mengineyo.

Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Ujumbe wa Madaktari Bingwa kutoka Jumuiya ya Kiislamu Duniani(WAMY)kuhusiana na matibabu watakayoyaendeshaKisiwani Pemba mazungumzo yaliofanyika katika Hoteli ya Mizingani Forodhani mjini Unguja.

 

Kiongozi wa Ujumbe wa Madaktari bingwa kutoka Jumuiya ya Kiislamu Duniani (WAMY) Dk,Sultan akizungumza machache kuhusiana na matibabu watakayoyaendesha wakati walipokutana nakufanya mazungumzo katika Hoteli ya Mizingani Forodhani mjini Unguja.madaktari hao watakuwepo kisiwani Pemba kutoa matibabu mbalimbali ikiwemo matatizo ya akina mama na mifupa kwa siku 10.

 

Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akipokea Zawadi ya Sahani baada ya kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Madaktari Bingwa kutoka Jumuiya ya Kiislamu Duniani(WAMY)kuhusiana na matibabu watakayoyaendeshaKisiwani Pemba mazungumzo yaliofanyika katika Hoteli ya Mizingani Forodhani mjini Unguja.