RAIS  Nicolás Maduro wa Venezuela amefichua kwamba, rais wa zamani wa Colombia ameajiri makumi ya mamluki waliopewa jukumu la kumuua yeye.

Nicolás Maduro amesema katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: “Njama hiyo ya mauaji ya Álvaro Uribe imekuwa ikifanyiwa kazi katika siku za karibuni, na mamluki 32 wameajiriwa kuniua mimi.”

Awali Maduro alisema  Marekani imeitaka Colombia itekeleze mpango wake wa kumuua Rais huyo wa Venezuela. Washington na Bogota zimekanusha matamshi hayo.

Jaribio la mwisho la kutaka kumuua Rais Nicolás Maduro wa Venezuela lilifanyika mwezi Agosti mwaka jana wakati kiongozi huyo alipokuwa kihutubia hadhara wa wanajeshi mjini Caracas. Hujuma hiyo ilijeruhi watu saba ingawa Maduro mwenyewe hakupatwa na madhara.

Wiki iliyopita kiongozi huyo wa Venezuela alitangaza kuwa anazo nyaraka na ushahidi unaothibitisha kwamba, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton, ndiye aliyepanga jaribio hilo lililoshindwa na kutaka kumua Rais wa Venezuela.