Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu kwa kuwasimamisha kazi Polisi 12 waliotuhumiwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Rais huyo mapema Jumatatu hii, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa kumuapisha Mkuu mpya wa majeshi, Luteni Jenerali Venance S. Mabeyo.

“Naomba nitoe pongezi kwa mkuu wa Polisi kwa kuwasimamisha kazi wale Polisi. Nikupongeze mkuu umefanya vizuri na umetoa heshima kwa nchi yetu, tembea kifua mbele, katika vita hii ya madawa ya kulevya hakuna cha mtu aliye maarufu atakayeachwa, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri, au watoto wa fulani ambaye akijihusisha aachwe,” amesema Rais Magufuli.

“Hata angekuwa mke wangu Janeth akijihusisha we shika tu, kwa sababu madhara ya madawa ya kulevya katika taifa letu imefikia mahali pabaya, haiwezekani watu wawe wanauza kama Njugu, sisi sote hapa tuliopo tunafahamu hii vita ni ya kila mtu,” ameongeza.