Rais Dkt John Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuwafukuza kazi mara moja watendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania(ATCL) watakaokwamisha ufanisi wa huduma za kampuni hiyo.

Rais Dkt Magufuli ametoa agizo hilo wakati wa uzindizi wa ndege mpya mbili za ATCL aina ya Bombardier zilizonunuliwa kwa fedha taslimu za kodi za wananchi kutoka Canada.

“Usimuonee huruma yeyote anakwamisha ufanisi wa huduma za shirika letu la ndege. Naona waziri unaangalia pembeni. fukuza kazi yeyote anayekweny kinyume cha kasi ya kusonga mbele kimaendeleo tunayoitaka,” amesisitiza Rais Magufuli.

Amesema shilingi Bilioni 100 zimetengwa kuanza ukarabati wa viwanja vya ndege nchini ili viweze kuhudumia ndege nyingi.

Aidha Rais Magufuli amesema kuna mpango wa kununua ndege nyingine mbili moja yenye uwezo wa kubebea abiria 160 na nyingine watu 240.