Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata amesema kuwa Mahakama ya Afrika Mashariki haina mamlaka kisheria kusikiliza hoja za kupinga uwepo wa Taifa la Tanzania lililotokana na Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. 

Wakili Malata amesema hayo leo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu usikilizwaji na uamuzi wa shauri namba 09/2016 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki baina ya Rashid Salum na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyosikilizwa jana Septemba 29, 2020.

Wakili Malata amesema kuwa Mahakama ilikubaliana na hoja hizo ambazo kwa mujibu wa mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Tanganyika na Zanzibar sio nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bali mwanachama wa jumuiya hiyo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo Novemba 2, 2016 Rashid Suleiman Adily na wenzake 39,999 walikwenda Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na kufungua shauri namba 09 ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu kiongozi wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.