Mahakama yatoa maamuzi ya mwisho, Baa 33 kuuza vileo Kaskazini Unguja

Wafanyabiashara ya vileo pamoja na Wamiliki wa baa Wilaya ya Kaskazini B Unguja wamesema wamefurahishwa na maamuzi ya Mahakama kwa kuwaruhusu  kuendelea na biashara ya Vileo kwa mwaka huu 2019.

Wakizungumza nje ya Mahakama baada ya kutolewa maamuzi hayo na Hakimu Mohamed Subeit kwenye Mahakama ya Mkoa Mfenesini wamesema  fursa hiyo waliyopewa ya kuendelea biashara  hiyo ya pombe,wameahidi kuitumia vizuri ili kuweza kuzalisha mapato ya serikali kwa wakati na wao kujikimu kimaisha.

Wamesema  wanaamini  utendaji wao wa  biashara hiyo ni mzuri ndio uliowasaidia   kupewa tena fursa ya kuendelea kuekeza kwenye maeneo ya biashara.

Kwaupande wake Katibu wa Vileo zanzibar Saleh Ali Abdalla amesema  mahakama imeridhishwa na utendaji kazi wa wafanyabiashara hao kwani wanafuata sheria zote za biashara hiyo lakini amewaasa kuendelea kuweka uwaminifu  na kufuata sheria zote pamoja na kulipa kodi za serikali kwa wakati.

Amesema miongoni mwa sababu iliyopelekea baa hizo kutokufungwa ni kwamba hakuna malalamiko  ya wananchi  waliojitokeza  kuzipinga mahakamani.

Amina Omar