Jumla ya mahujaji 2,500 kutoka Tanzania wanatarajia kuondoka nchini kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza ibada ya hija ambayo ni nguzo ya tano ya uislamu.

Mahujaji hao ni wale kutoka taasisi 37 zilizosajiliwa na kukamilisha vigezo ikiwemo 22 kutoka Zanzibar na 15 kutoka Tanzania Bara, kati ya taasisi zaidi ya 40 zilizopo Tanzania.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Kitengo cha Dini kutoka Kamisheni ya Wakfu na Maliamana Zanzibar, Khalid Mohammed Mrisho, ofisini kwake Mazizini.

Alisema, mahujaji hao 1,700 ni kutoka taasisi zilizosajiliwa Zanzibar na 800 kutoka Tanzania Bara.

Aidha, alisema mahujaji wa mwanzo kutoka ni kutoka taasisi ya Zadawa ambayo itaondoka nchini Julai 24 mwaka huu na mahujaji wa mwisho kurejea nyumbani ni wale wanaoondoka na  taasisi ya Ahlusafari.

Mahujaji hao watarejea Septemba 29 mwaka huu.

Aliwaomba wananchi hasa vijana wenye uwezo kwenda hija wakiwa na nguvu na sio kusubiri wakiwa wazee.

Aliwasisitza mahujaji kujitahidi kujifunza ibada hiyo na kutekeleza ibada wakiwa na maarifa na kufuata taratibu zilizowekwa.